SERIKALI inapoamua kutengeneza mswaada wa sheria na baadaye kuuwasilisha katika chombo chenye jukumu la kutunga sheria, huwa imefanya utafiti wa kutosha na kujiridhisha kwamba uwepo wa sheria hiyo utakuwa msaada mkubwa kwa jamii.

Haijapata kutokea na kama imetokea basi ni sehemu nyengine ya dunia, si Zanzibar kwa serikali kukurupuka kutengeneza sheria isiyo na kichwa wala miguu na kuipeleka kwa wananchi.

Kabla ya serikali kuandaa mswada wa sheria, lazima iwe imefanya utafiti na kubaini tatizo liliopo utatuzi wake unahitaji sheria ili kuzuia, kulinda ama kuhifadhi kitu ambacho kina umuhimu mkubwa kwa maslahi ya jamii.

Jambo jengine muhimu katika kuinasibisha sheria hiyo na jamii, serikali huyashirikisha kikamilifu makundi husika kutoa maoni na michango itakayosaidia kuifanya sheria hiyo iwe bora na kutekelezeka kwa urahisi.

Tunafahamu vyema sheria wanazotunga wanaadamu haziwezi kuacha kuwa na kasoro, kwa sababu mwanadamu mwenyewe ni kiumbe dhaifu na ametolewa kasoro kadhaa na muumba wake.

Sisi hatuna matatizo na sheria zetu zinazotungwa hapa Zanzibar, na tunathubutu kusema kuwa visiwa hivi vimejaaliwa kuwa na sheria nzuri na za kupigiwa mifano.

Sheria tulizonazo zimekuwa nzuri kwa sababu mbalimbali ikiwemo ile ya kufanyiwa utafiti wa tatizo liliopo na ushirikishwaji wa jamii wakati wa kuundwa kwa sheria hizo.

Kitu chengine cha kufurahisha ni kwamba, sheria zetu nyengine zina viwango vya kimataifa na kwamba yale yaliyopo hapa kwetu tuliyoyatungia sheria, hayana tofauti na nchi za wenzetu.

Pamoja na mazuri hayo, tatizo letu ni utekelezwaji wa sheria hapa Zanzibar, suala hilo limekuwa changamoto kubwa inayoturejesha nyumba na kutofikia maendeleo ya kijamii, kiuchumi wakati mwengine watu hata kupoteza maisha kwa ukaidi tu wa kutofuata sheria.

Labda tutoe mfano mdogo tu tena wa kawaida sana, hivi kuna tatizo gani kwa mtu anayeendesha chombo cha magurudumu mawili kupandia chombo hicho bila ya kuvaa kofia ngumu?

Sheria inaeleza wazi kuwa mtu anayeendesha chombo hicho avae kofia hiyo, wakati mwengine dereva hakuvaa kofia hiyo na hata mtu aliyepewa lifti naye hakuvaa.

Kama mfano huo hautoshi, mwengine ni ule wa sheria ya kuvaa ukanda unapopanda gari, hili nalo lina ubaya gani ama utaathirika nini kama utauvaa ukanda huo ukiwa kwenye gari?

Wakati mwengine polisi usalama barabarani wanapofanya wajibu wao kumkamata mtu aliyekwepa sheria, hutokezea wakubwa waliovaa makoti na yaliyolizidi gwanda la polisi kimamlaka kutaka ndugu ama jamaa yake aachiliwe.

Lakini pia aliyekamatwa naye hupapatua na kufanya kila aina ya ushawishi wa kutoa rushwa ili kukwepa kupelekwa mahakamani, kwa kile anachoeleza kuwapelekwa mahakamani ni aibu.

Hivi mambo haya ya kiujomba, kiushangazi, kiudugu, kimuhali yataisha lini ama dawa yake tutaipata wapi ili tuachane nayo.

Mathalan inapotokezea ajali kuwa hukuvaa ukanda ama kofia ngumu, athari huwa kwa polisi anayesimamia utekelezaji wa sheria ama kwako wewe aliyetundika miguu hospitali ya Mnazimmoja.

Tunapaswa kujipanga upya ili kuhakikisha jamii inawajibika kwenye kila utekelezaji wa sheria, lakini isiwe utekelezaji huu kwa wadogo, huku wakubwa wakitumia nafasi zao kujifanya wako juu ya sheria.

Haipendezi viongozi, ndugu na jamaa zao kuwa vinara wa kukiuka sheria kwa sababu tu ya ukubwa, hali hiyo inarejesha nyuma morali ya utendaji kazi ya jeshi la polisi katika kusimamia sheria.


Ifikie wakati polisi waache rushwa na wanaokamatwa waache kushawishi rushwa, ili kila aliyevunja sheria akawajibike, kwani utekelezaji wa sheria zetu kikamalifu ndiko kutakako tuwezesha kupiga hatua za kimaendeleo.