KAMA kuna zawadi kubwa na muhimu kabisa tuliyopatiwa na Mwenyezi Mungu sisi watu wa Zanzibar, Tanzania, Afrika Mashariki na Kati ni tunu ya kipekee ya lugha ya Kiswahili.

Wageni walipo tawala sehemu mbalimbali duniani walilazimisha kuzungumzwa kwa lugha zao, ndio maana hatushangani maeneo mengi duniani yamekuwa yakizungumzwa lugha za kikoloni hadi leo.

Na kwa jinsi wakoloni walivyokuwa washindani, ambapo hivi sasa huitwa mataifa makubwa wakazivisha hadhi lugha zao na kuziita lugha za kimataifa, ambapo kila mkutano muhimu duniani mawasiliano ni kupitia lugha zao.

Kwa jinsi walivyozitukuza lugha zao, wametulazimisha na kutuaminisha kuwa ufasaha wa kuzitumia lugha zao kwenye kuzungumza na kuandika ndio upeo wa utaalamu.

Pamoja na kwamba sehemu ya mwambao wa Afrika Mashariki ilitawaliwa na wakoloni kwa miaka kadhaa, lakini watu wa eneo hili hawakuweza kusahau lugha ya Kiswahili waliyozaliwa nayo.

Kiasili hasa lugha hii ilianzia pwani ya Afrika Mashariki na kusambaa katika nchi kadhaa zilizokaribu na pwani hiyo hadi kuelekea sehemu za bara arabu na duniani kote.

Viko vyuo vikuu kutoka nchi mbalimbali duniani vinafundisha lugha ya kiswahili baada ya kutanabahi umuhimu wa lugha hiyo, ambapo baadhi ya vyuo hivyo vinatoa shahada za juu kabisa.

Aidha vipo vyombo vya habari vya kimataifa hasa redio zinazo peperusha matangazo yao kwa kutumia lugha ya Kiswahili, mafanao wa redio hizo ni kutoka nchi za China, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Japani, Uturuki, Iran na kadhalika.

Hata hivyo ukweli ni kwamba Kiswahili hivi sasa kinapita kwenye wakati mgumu, ambapo nyumbani kwao ndio kimeanza kupoteza hadhi katika nyanja mbalimbali.

Kwa mfano, wazungumzaji wa Kiswahili hivi sasa tunawazungumzia wa hapa Zanzibar ambapo inaamika lugha hii ndio kwao, wameanza kutamka sivyo baadhi ya misamiati.

Aidha hali imekuwa mbaya sana hata kwenye maandishi Kiswahili kinaandikwa ndivyo sivyo, mambo yanachanganywa na kupandiana, kwa mfano leo hii Zanzibar muandishi anaandika ‘watu nane’ badala ya watu wanane dada anaitwa mdada! na kaka anaitwa mkaka, ujumbe wingi wake unalazimishwa na kuitwa jumbe!

Kwenye vyombo vya habari huko ndiko hakusemeki, ripoti za waandishi ziko shaghala baghala, ukiuliza utaambiwa mtangazaji ni mzaliwa halisa wa Zanzibar.

Haipendezi kuorodhesha vyombo vya habari vya Zanzibar vyenye kuiharibu lugha hii ama kwa makusudi ama kwa kutokujua, lakini tukubali tu kuwa hali imekuwa mbaya sana na kama ni mgonjwa yuko wodi mahututi.

Hatushangai sana kwa vituo vya habari vya nje ya Zanzibar kuchukua kila kitu hata wakati mwengine kuingia kwenye mamlaka ya kutohowa hata kama si jukumu lao na kutumia kila kichaotoholewa hata kama si rahisi.

Vyombo vyetu navyo vimeingia kwenye mkumbo wa kuiga kila kinachotoholewa hata kama maneno mengine yanayotoholewa kutakwa mbele za watu ni karaha.

Kwa mnasaba huo vyombo vya habari tuhakikishe tuwe wa kwanza kwenye matumizi sahihi ya lugha ya kiswahili na pale tunapokwazika Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), lipo kwa ajili ya kutusaidia.

Aidha BAKIZA wapewe nguvu kuyakataa maneno yanayotoholewa nje ya nchi ambayo wakati mwengine yanaukakasi hata kuyatumia mbele ya kadamnasi.

Aidha tuache tabia za kuandaa mikutano kwenye chumba kuwa na wazungu wawili waswahili 50, halafu tunalazimisha kuzungumza lugha za kikoloni.

Lazima tufahamu kuwa Kiswahili lugha yetu, Kiswahili utamaduni wetu, Kiswahili tunu yetu hivyo tukitunze na tusikiharibu.