WAWAKILISHI wa Zanzibar katika michuano ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF),Mlandege na KVZ, leo na kesho wanatarajiwa kushuka uwanjani kusaka tiketi ya kufuzu hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Kwa upande wa Mlandege ambao ndiyo mabingwa wa Zanzibar, watashuka kwenye uwanja wa Amaan kumenyana na CS Sfaxien ya Tunisia wakati KVZ watakaribishwa na El Amal ya Sudan.
Tunachukuwa nafasi hii kuzitakia kila la heri timu hizo ziweze kushinda katika michezo yao ya kwanza ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya pili.

Sote tunaelewa kuwa patashika za michuano hiyo ni ngumu na zenye kuhitaji maandalizi katika kukabiliana nazo na hilo tunaamini limefanyika kwa wawakilishi wetu hao.
Kutokana na hali hiyo, ni imani yetu kwamba wana kila sababu ya kushinda hasa ikizingatiwa wakiwa nyumbani watakuwa wakiungukwa mkono na Wazanzibari na hali hiyo ni moja katika njia ya ushindi ikizingatiwa mashabiki ni chachu ya ushindi.

Kwa kipindi kirefu, ushiriki wa timu za Zanzibar kwenye michuano ya Afrika haujakuwa mzuri na kumekuwepo na dhana iliyojengeka miongoni mwa mashabiki kuwa timu zetu haziwezi kuvuka raundi za mwanzo za mashindano ya kimataifa.

Hivyo, tunawashauri wachezaji wa Mlandege na KVZ watambue kuwa wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kurudisha imani za mashabiki na kuondoa dhana hiyo potofu.

Na hilo litaweza kuondoka kwa ushindi pekee ambao utachangiwa na nidhamu ya mchezo wakati wote wa mashindano sambamba na wajibu wa kujituma mchezoni kwa wachezaji.
Zanzibar Leo tunaamini wachezaji na benchi la ufundi la Mlandege na KVZ watapeperusha vyema bendera ya nchi katika michuano hiyo na hatimaye kusonga mbele.

Kama ambavyo tunatarajia kuona ushindani katika michezo hiyo, hali ya kucheza kwa bidii na jihadi inatakiwa ionekane katika mechi zote ambazo watashuka uwanjani.
Kubwa tunalowaambia ni kwamba mnakwenda kwenye michuano hiyo kwa niaba ya Wazanzibari wote na hivyo mnatakiwa kupambana.

Mbali na kuiletea nchi sifa, michuano hiyo ni nafasi nyengine kwa wachezaji wa Zanzibar kutangaza vipaji vyao na hatimaye kuzivutia klabu mbalimbali za nje ili kuwasajili.

Kufanya vizuri kwa timu za Zanzibar kwenye mashindano hayo kutarejesha imani ya mashabiki wa soka nchini baada ya kipindi kirefu cha kuondolewa mapema sambamba na kukosa aina fulani ya ushindi kama yalivyo mataifa yanayoinukia kwenye mchezo huo.


Hivyo tunawatakia kila la heri Mlandege na KVZ huku Wazanzibari tukiwa tupo nyuma yenu.Hivyo tunawatakia kila la heri Mlandege na KVZ huku Wazanzibari tukiwa tupo nyuma yenu.