NA MWANTANGA AME

DISEMBA 1 ni siku ya Ukimwi Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka, Zanzibar kama sehemu ya dunia nayo huadhimisha siku hiyo hasa kutokana na kuwa na watu walioambukizwa virusi hivyo hapa visiwani.

Wakati siku hii ikiadhimishwa hapa kwetu visiwani Zanzibar tayari imeonekana athari kubwa ya maradhi haya kuwakumba zaidi wanawake kuliko wanaume kutokana na sababu mbali mbali za shughuli za kijamii.

Kwa mujibu wa Meneja wa kitengo Shirikishi cha Ukimwi, Homa ya Ini, Kifua Kikuu na Ukoma, Dk. Farhat Khalid, alisema kwamba mwaka 2018 mpaka 2019 watu wanaoishi na VVU walikuwa ni 6,889, kati yao wanaume ni 2,146 na wanawake ni 4743.

Vile vile, alieleza kwamba watu 6,800 walikuwa wanaendelea kutumia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI kato yao wanawake ni 4,689 na wanaume ni 2,111.

Mbali na ongezeko hilo la asilimia 0.4. Dk. Farhati alisema mama wajawazito wenye maambukizi ya VVU ni asilimia 0.6, makundi maalumu kama vile wanaume wanaojamiana ni asilimia 5, wanaojidunga shindano za dawa za kulevya ni asilimia 5.11 na wanawake wanojiuza (madadapoa) ni asilimia 12.1.

Hali hii, inaonesha wazi kuwa kiwango cha wanaopata maambukizi ya maradhi haya bado wanawake wanaongoza, ikiwa ni kutokana na sababu mbali mbali, kwani hata kiwango cha dunia nacho imeonekana kundi hilo ndilo linaloongoza kwa ugonjwa huo.

Kwa upande wa kidunia idadi ya watu walioambukizwa na virusi vya ukimwi duniani kote inakaridiwa kufika Millioni 37.5. Lakini kinyume na miaka 10iliyopita ambapo wengi wa walioambukizwa walikuwa wanaume, leo kati ya wagonjwa wawili, mmoja ni mwanamke ambao ni maambukizi mapya.

Pamoja na hali hiyo, lakini bado wataalamu wa Umoja wa Mataifa hawana ujuzi mkubwa juu ya athari kwa wanawake na vilevile hawana mbinu maalum ya kuwasaidia na kuwalinda wanawake.

Wanachoweza kusema ni kwamba mbinu zinazotumika hadi sasa kupunguza kuenea kwa maradhi ya ukimwi hazitoshi zikiwemo zile za kuwapa ushawishi wa kutumia mipira ya kinga.

Lakini bado athari za kupata maambukizi kwa wanawake imeonekana kuwa kubwa kutokana na vitendo vinavyoendelea hivi sasa vya udhalilishaji kuongezeka na kinga hizo hazijamsaidia mtoto wa kike na ndio maana namba yao inaongezeka siku hadi siku.

Aidha jambo jengine linalopelekea wanawake kuwa waathirika wakubwa wa ugonjwa huu ni wasichana wa umri mdogo na wa kati bado wanakabiliwa na jinamizi na vitendo vya ubakwaji kwani wamekuwa wakilazimishwa kufanya ngono bila ya kupenda na kuingiliwa kwa nguvu.

Imeelezwa kuwa ongezeko hilo linachangiwa zaidi na utoaji wa elimu hivi sasa kuyalenga makundi fulani kama makahaba au madereva wa malori na jengine ni walio katika ndoa kutokana na kuwa hawana usemi juu ya waume zao wa kutaka kujua wanafanya mapenzi na nani.

Kutokana na hali hiyo, ndio maana haishangazi kuona kundi hili idadi yake linakuwa zaidi, na maambukizo ya maradhi haya, licha elimu imekuwa ikitolewa, kwani wengi wanajikuta kutoa somo hili bado wanaliangalia kundi la watu wanaoishi mjini kuliko vijijini.

Leo hii, Zanzibar kwa mujibu wa ripoti ya Mtakwimu Mkuu wa serikali imekiri kwamba  za waathirika na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kubakwa vimeongezeka , kwani kipindi cha mwaka 2019  matukio 1,369 yaliripotiwa katika vituo mbali mbali vya Polisi, ambapo matukio hayo 651 ni ya ubakaji, 157  kulawiti, 269 Shambulio na yaliyobakia ni kutorosha na kukashifu.

Hata hivyo, ripoti hiyo imeeleza kwamba katika mwezi wa Oktoba mwaka huu, matukio 103 yameripotiwa katika vituo vya Polisi, ambapo kati ya matukio hayo 16 ni wanawake na 87 ni ya watoto.

Hali hiyo ikiwa bado inatisha, inafurahisha kumsikia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, kuvishupalia vitendo hivyo, kwa kuwataka walipoewa majuku kuona wanasimamia vyema kuzuiya matendo hayo yasiendelee.

Hivyo basi, ipo haja ya kuona umuhimu wa kulifanyia kazi suala hili, ili kuwaokowa wanawake kuongeza idadi ya wanaoathirika na maradhi haya, kwani mbinu ya kupambana na ukimwi zibadilishwe kabisa kwa kuwa na suluhisho linalozingatia kipindi kirefu kwa kulazimisha kuzibadilisha sera ziliopo sasa.

Nafikiri jambo kubwa ni kwamba maradhi ya ukimwi yasitumiwe kwa sera za dharura tu, bali tutambue kwamba virusi hivyo vitakaa nasi duniani kote na wakati wote.

Hivyo, wakati umefika sasa kuangalia sera na sheria zitazodhibiti njia za kuongezeka maradhi haya kwa kuukataa udhalilishaji hasa ubakaji, ili tuache kuikumbusha jamii kila ifikapo Disemba 1, ya kila mwaka.