Sayansi na teknolojia huchangia hali hiyo

Na Maria Inviolata

MITINDO ni sehemu ya utamaduni ambao ni jinsi binadamu anavyokabili maisha katika mazingira yake, hivyo hujumuisha ujuzi, imani, sanaa maadili, sheria, mila na desturi  ambavyo mtu hutenda na kupata kama mwanajamii.

Pia utamaduni ni sifa maalumu inayomtofautisha mwanadamu na wanyama, utamaduni ni suala la msingi katika anthropolojia, ukihusisha yote yanayorithishwa katika jamii fulani, kama vile lugha inayounganisha wahusika, mavazi, fasihi, mafungamano, ndoa, michezo, ibada, sayansi na teknolojia.

Utamaduni ulioendelea ambao hivi sasa unatawala dunia unaitwa “ustaarabu au usasa wa kimagharibi”. Utamaduni unabadilikabadilika ndani ya watu, baadhi wanachangia na kuunga mkono mabadiliko hayo, wakati wengine wanayapinga. Ujuzi mpya na teknolojia, pamoja na mahitaji ya uchumi, ni kati ya mambo yanayosukuma zaidi kubadili kwa utamaduni.

Mitindo ina nafasi kubwa ya kukuza au kupotosha utamaduni husika ambao hutumiwa na kikundi au jamii kuwasilisha jambo kwa namna maalum, kwa mfano kufanya jambo haraka haraka au polepole kwa taratibu fulani, hiyo namna maalum huenea katika jamii  hasa upande wa mavazi. 

Mitindo hubadilika badilika kadiri ya mahali na nyakati, hiyo namna kubadilika ni njia rahisi ya  kuenea hadi  kupotosha utamaduni kupitia ubunifu wa mitindo.

Matamasha ya mitindo yanayoandaliwa duniani hivi sasa yanakabiliwa na upinzani juu ya utunzaji wa utamaduni. Baadhi ya wabunifu na waandaaji wa mitindo huchukulia nafasi hiyo kuwa ni nafasi ya uhuru wa kujieleza,  Je, Ni kweli matamasha hayo  hayapotoshi tamaduni za nchi nyingine?

Hilo ni swali ambalo limekuwa likitatiza watu wengi juu ya mitindo na utamaduni.

Kuna watu maalumu ambao wanabuni mitindo mipya, wanaionyesha na kuisambaza, mara nyingi watu hao hutumia njia hiyo kwa faida zao za kiuchumi, kutokana na utandawazi siku hizi mitindo inaenea duniani kote kwa haraka hasa kutoka nchi tajiri kwenda nchi maskini, na pengine huharibu maadili na utamaduni wa nchi nyingine.

Maendeleo nayo yamekuwa yakiathiri tamaduni za makabila au jamii ya watu wa nchi nyingi, mathalani habari kubwa zilizoshika hatamu duniani ni ile ya Serikali ya Mexico kumshutumu mbunifu wa maarufu mwanamitindo Carolina Herrera kwa kupotosha utamaduni wa nchi hiyo.

Msemaji wa Bi Herrera, alisema kuwa alama ya lebo ya mbunifu huyo mzaliwa wa Venezuela inatambua kazi za wafanyabiashara wa Mexico na utamaduni asilia wa nchi hiyo na kuongeza hivi:  

Mkusanyiko uliotumiwa na mbunifu huyo uliongozwa “Na rangi tajiri za nchi hiyo na ujuzi asilia  wa Kimexico”  shirika la la habari la AP lilimnukuu msemaji huyo wa Herrera kuhusu vazi hilo lilioleta mzozo.

Pamoja na suala hilo kutolewa ufafanuzi, Katibu wa utamaduni wa Mexico aliiandikia barua rasmi nyumba ya mtindo  ya nchi hiyo akilalamika kuhusu matumizi ya mifumo  ya asili ya mitindo na utamaduni wa jamii asilia  za Kimexico jinsi ulivyopotoshwa na mbunifu huyo Bi Hereila.

Wakati hayo yakijiri mbunifu mwingine wa mavazi Kim Kardashian West aliingia katika malumbano na wananchi wa Japan, Kim aliwaudhi Wajapani kwa kuanzisha mtindo wake wa vazi la kimono linalobana maumbile ya mwili, na kulibatiza “Kimono Intimates”. Kimono ni vazi la kitamaduni la Japan la karne nyingi, wataalamu wa Japan wanasema kuwa nguo ya Kimomo ya ndani haifanani na kimono cha kitamaduni cha Kijapan, Lakini wajapani kwenye mitandao ya kijamii walisema kuwa nembo hiyo ni kulikosea heshima vazi lao la kitamaduni na la kitaifa.

Matukio kama hayo siyo mageni nchini Tanzania, baadhi ya wabunifu na waandaaji wa mitindo nchini walipingwa na watu wengi kwa kupotosha uvaaji wa vazi la Kanga kwa  mitindo tofati  ya uvaaji  vazi hilo ambalo huvaliwa kwenye sherehe za aina mbali mbali kama vile, Harusi, misiba, sherehe za kimila, Kidini, malezi, Kitaifa na shughuli nyingine za mapishi, kilimo, mavuno , hata kutupia begani kanga moja iliyokunjwa kitaalam ilihali umevalia Kimagharibi.

Mhadhiri katika Idara ya sanaa bunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dkt. George Nahimiani, anasema kuwa baadhi ya wabunifu wa mitindo ya mavazi ambao ni sehemu ya wasanii na wanamuziki wa kike hapa nchini kwa kiasi fulani wanachangia upotoshaji wa mavazi yanayoakisi utamaduni wa mavazi ya jamii ya watu wa nchi hii, hasa kwa upande wa mavazi.

Mtaalamu huyo wa sanaa anafafanua hivi : Wabunifu wa mitindo ya mavazi wana dhima kubwa ya kubuni mitindo mbalimbali ya mavazi kama taaluma yao inavyowaelekeza,  taaluma bunifu inakuwa kwa kasi na kuwa moja ya ajira na inainua pato la wabunifu na kuchangia pato la taifa.

Kwa bahati mbaya kwa hivi sasa, kuna kila dalili ya dhima ya taaluma hiyo kupotoka hasa pale kile kinachobuniwa kisipolenga soko la ndani ambalo linaheshimu mila desturi na tamaduni ya jamii ya watu na kuegemea zaidi katika mtazamo na matakwa ya soko la nje ambalo halifungwi na tamaduni ya nchi atokayo mbunifu bali hulenga soko na pato la mbunifu zaidi.

Inapofikia hapo ndipo kelele za wanajamii wanaothamini mila desturi na utamaduni wao zinapojitokeza.

Aliendelea kutoa mfano wa mavazi yanayoonekana yakitumiwa na baadhi ya wasanii wa muziki wawapo kazini ambayo kitaalamu yanaitwa ‘Maleba’, kihalisia ‘Maleba’ ni vazi rasmi lililoandaliwa na kuvaliwa na msanii yeyote yule pale tu anapowajibika katika taaluma yake.

Maleba siyo vazi rasmi nje ya maisha ya msanii isipokuwa pengine pale tu anapoamua kulitumia kama sehemu ya kujitangaza nakadhalika.

Mtaalamu huyo anafafanua  hivi: baadhi ya wasanii wameonekana wakiwa wamejipamba kwa mavazi ambayo utadhani anatamani aliondoe tu na abakie mtupu,  bahati mbaya teknolojia imerahisisha na kuwafanya waweze kuonekana kwenye picha za mnato au kwenye televisheni na mitandao kadhaa ya kijamii,  bahati mbaya kwa kuelewa au kutoelewa baadhi ya wanajamii wanapoona hivyo  kwa mfano mwanamuziki amevaa Kimaaleba, kwa kutambua au kutotambua kuwa vazi hilo ni Maleba, mwanajamii naye akaenda kutengeneza vazi hilo  Maleba na kulivaa kama vazi la kawaida!

Kinachotokea ni jamii kumwona mbunifu na msanii kuwa wamechangia kumpotosha mwanajamii kimavazi, dhana ambayo huenda siyo dhamira ya mwanamitindo wala msanii.

Mwanazuoni huyo anahitimisha kwa kuhoji hivi: lazima Msanii avae vazi Maleba la nusu Uchi? Ile dhana ya msanii ni kioo cha jamii inahusu ujumbe tu? Maleba siyo sehemu ya kioo cha jamii? alihitimisha kwa kushauri hivi: “Yapo baadhi ya Maleba ambayo kulingana na aina ya shughuli iwe ni  sanaa au aina ya mchezo yanakubalika.

“Kwa mfano vazi la mchezo wa kuogelea, sarakasi, riadha, mpira wa pete nakadhalika kwa kufuata misingi ile ile kwamba Maleba hayo yasivaliwe nje ya maeneo yanakotumika rasmi,  hayo tunayooneshwa sasa kupitia televisheni na mitandao ya kijamii ni ishara tosha kuwa sanaa ya ubunifu mitindo hapa nchini inaingiliwa na tamaduni za ughaibuni na msukumo wa soko la nje ambalo watumiaji wake linawajumuisha wanajamii ambao siyo utamaduni wao”, anasema.

Anafahamisha kuwa kama lilivyo vazi la Kanga, Kimono ni vazi la kitaifa la Japan, ambalo huvaliwa katika matukio maalumu. “Tunavaa vimono tukiadhimisha afya, ukuaji wa watoto, harusi, mahafali, katika mazishi. Ni nguo ya sherehe na hurithishwa kwa familia kupitia kizazi hadi kizazi,” mmoja wa wanawake wa Japan Yuka Ohishi alipozungumza na BBC na kufafanua hivi: “Hii nguo ya kubana maumbile haifanani na kimomo  hata kidogo-ameamua tu kuchagua neno ambalo lina ‘Kim’ ndani yake – hakuna heshima kwa maana ya utamaduni wetu wa vazi, vazi hilo la Kimono lililoanza kuvaliwa nchini Japan katika karne ya 15.

Naye Profesa Sheila Cliffe akitofautisha nembo Kimono cha Kim West ambaye pia ni nyota wa kipindi cha maisha halisi nchini Marekani anasema kuwa nembo ya Kimono ca Kjapani ni ya kipekee kwa ajili ya “kusherehekea na kusitiri umbo la mwanamke “. Kimono huvaliwa na mwanamke ili kuzuia mwili wake usionekane.

“Umaana wa kimono ni baraka, nadhibu na upole, hakimaanishi kuonyesha umbo au kubana- umbo, humfunika mvaaji ili kusitiri umbo lake,” alifafanua Profesa Sheila Cliffe kutoka Chuo kikuu cha wanawake cha Jumonji alipozungumza na BBC na kusema hivi: “Kama nikitengeneza sidiria na nikaita sari… baadhi ya watu wataudhika sana, inaonyesha ukosefu mkubwa wa heshima … Kimono inaelezea utambulisho wa Wajapan. Hilo neno si la Kim Kardashian.”

Hata hivyo mmoja wa wataalamu wa kimono anasema ni wazi Kimono kinatambuliwa chenyewe kwa nguo ambazo ni kinyume na nguo ya kubana maumbile.

Watu wengi wamelichukulia suala hili kwa uzito mkubwa kwasababu alitumia jina la nembo ya nguo yenye maana kubwa kwa utamaduni wa Wajapan, kinachokera zaidi ni kwamba nguo ya kitamaduni sasa ina jina sawa na nembo ya nguo ya ndani, baadhi wanahofia watu wataanza kuhusisha kimono cha Kim Kardashian West, badala ya Kimono asilia cha Japan.”Ninadhani Kim ana ushawishi mkubwa katika utamaduni wa pop, ninahofu  kutakuwa na watu ambao wanafahamu jina kimomo pekee kama nembo yake,”alisema Bi Ohishi.

Historia ya vazi hilo inamuhusisha mtu mmoja anayetajwa kwa jina moja tu la ‘Mo’ aliyelibuni vazi hilo kutoka kwa mtu mwingine aliyevaa aproni juu ya vazi lingine katika miaka ya 1336–1573.  Vazi hilo la Kimono linatajwa kuwa asili yake ni China.

Hata hivyo Kim Kardashan amefuta jina hilo la Kimono katika vazi lake la kubana la kusherehekea umbo la mwanamke.