ADISS ABABA, ETHIOPIA

WAZIRI mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameuambia ujumbe wa Umoja wa Afrika kwamba ataendeleza operesheni ya kijeshi katika jimbo la Tigray.

Waziri mkuu huyo aliendelea wito wa mazungumzo huku vikosi vya serikali vikiendelea na awamu ya mwisho ya mashambulizi dhidi ya vikosi vya jimbo hilo.

Hapo juzi waziri mkuu huyo aliupokea ujumbe wa viongozi wa zamani kutoka mataifa matatu ya Afrika, Joaquim Chissano wa Msumiji, Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia na Kgalema Motlanthe wa Afrika Kusini, waliotumwa na Umoja wa Afrika kama wasuluhishi.

Kwenye taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo, Abiy alisema ameridhishwa na hatua hiyo, inayoashiria dhamira thabiti ya mataifa ya Afrika katika kusuluhisha migogoro ya Afrika.

Hata hivyo, alisema kuwa serikali yake ina mamlaka ya kikatiba ya kutekeleza sheria katika jimbo hilo na kote nchini Ethiopia.

Serikali ya Tigray kwa upande wake imesema jana kwamba vikosi vya serikali vimeshambulia kwa mabomu miji na vijiji na kusababisha uharibifu mkubwa, ingawa haikuutaja mji wa Mekele.