WATU wengi wanasema kobe anajificha ndani ya gamba lake ili kujilinda, lakini   ripoti mpya iliyotolewa na kikundi cha utafiti wa viumbe vya kale kimetoa taarifa mpya kuhusu kobe kuwa na gamba.

Matokeo ya watafiti hao yamebainisha kuwa kobe walipata magamba ili  kuendana na mabadiliko ya mazingira na kwamba lengo halikuwa kujilinda, bali ni kuchimba chini ya ardhi.

Wanabiolojia wanasema kobe aina ya ‘Eunotasaurus’ walioishi nchini Afrika Kusini katika miaka milioni 280 iliyopita, huenda ni mababu wa makobe wa kisasa.

Uchambuzi wa mabaki ya kobe wa kale na mchakato wa ukuaji wa gamba la kobe wa kisasa wote unaonesha kuwa gamba hili ni mbavu zilizopanuliwa.

Kobe wa kale wana mbavu pana, ambazo bado hazijaunganishwa pamoja na kuunda gamba.

Watafiti wamegundua mabaki kadhaa ya kobe wa kale katika bonde la Karoo nchini Afrika Kusini, ambapo moja limehifadhiwa vizuri na linaonesha mifupa kamili ya kobe.

Watafiti wamesema katika miaka milioni 250 iliyopita, viumbe vingi vilitoweka, lakini kobe aina ya ‘Eunotasaurus’ walinusurika.

Huenda wakati huo kobe hao walijitahidi kuchimba chini ya ardhi ili kukimbia mazingira mabaya juu ya ardhi.

Ili kuhakikisha mikono yao inachimba kwa nguvu kubwa, kobe hao walihitaji kuwa na miili imara. Katika hali hii mbavu zao zilipanuka hatua kwa hatua na mwishowe kuunda gamba.