NI siku chache zimepita tangu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alipoteua na kuliapisha baraza la mawaziri la awamu ya nane.

Katika baraza hilo kuna mchanganyiko wa mawaziri wakongwe, wenye uzoefu pamoja na vijana ambao hawana uzoefu sana ya kiutendaji kwa nafasi kama hiyo kubwa na hata kisiasa.

Ndani ya muda huu mfupi, tumewaona mawaziri wakipigana vikumbo mabarabarani, wakipishana kutoka na kuingia katika ofisi na taasisi zao, wakiwa wanafanya ziara rasmi za kujitambulisha na kuzielewa taasisi zilizochini ya wizara zao.

Katika kipindi hicho kifupi cha mawaziri kufanya ziara katika idara na taasisi zao na kupata fursa ya kuzungumza na wafanyakazi, tumeshuhudia yakiibuka mengi na mengine kwa hakika ni ya kushangaza sana, huku yakizua masuali mengi bila ya majibu.

Lakuvutia lakini si la kuvuatia kama lilivyo bali ni la kusikitisha lililojaa kwenye mitandao ya kijamii na kusababisha gumzo ni suala la meli ya MV. Mapinduzi II, ambapo baada ya waziri wa wizara hiyo kuitembelea meli hiyo amebaini manyago.

Kwa mujibu wa taarifa za mhandisi alizozitoa mbele ya waziri, meli hiyo iliyotengenezwa nchini Korea Kusini kwa gharama ya kibunda cha dola milioni 30.4, mashine zake zote ni mbovu tangu ilipowasili visiwa hapa.

Aidha mhandisi huyo alibainisha kuwa mashine za meli hiyo hazizimwi moto, kwani endapo zitazimwa, zinaweza zisiwake tena na huo ndio ukawa mwisho wa maisha ya meli hiyo kubwa yenye uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na mizigo tani 200.

Na kwa mujibu wa kaimu mkurugenzi wa shirika la meli, ni kwamba kwa sababu meli hiyo mashine zake hazizimwi moto, kwa siku moja kwa maana ya kipindi cha saa 24, meli hiyo inatumia shilingi milioni nne kwa ajili ya mafuta.

Hapa nataka uelewe kuwa mafuta hao ya milioni nne yanayotiwa kila siku sio ya kuifanya meli hiyo itekeleza majukumu yake ya kusafirisha abiria na mizigo, bali mafuta hayo ni kwa ajili ya kuwashia mashine tu ili kuepuka meli kuzima na kufikia mwisho wa maisha.

Kiukweli hizi ni taarifa sio za kushangaza tu, lakini ni za kusikitisha sana kwani lengo la serikali kuinunua meli hiyo lilikuwa ni kuwapunguzia adha ya usafiri wananchi wa Unguja na Pemba, lakini lengo hilo limeshindwa kufikia.

Kwa ufupi kabisa kuendelea kuwepo kwa meli hiyo kunawatia hasara sana wananchi wa Zanzibar na hatudhani kama tangu ilipofika kwa safari chache ilizozifanya gharama za dola milioni 30.4 zimerudi.

Pamoja na kwamba kuna masuali mengi kwa sasa kwa wananchi wa Zanzibar kuhusiana na meli ya Mapinduzi II, tunaamini serikali itatumia busara kulimaliza sakata hili la mapinduzi II ambayo ni mali ya wananchi wa Zanzibar.

Wengine tunakumbuka vyema wakati serikali ilipofikia uamuzi wa kuwa na meli mpya ya abiria na mizigo, ofisi nyingi kazi za kawaida zilishindwa kufanyika kutokana na fedha za OC kuelekezwa kwenye ununuzi wa meli hiyo.