MNAMO Novemba 28 mwaka huu wizara ya ulinzi ya Iran ilitoa taarifa za kifo cha mmoja wa wanaoaminika kuwa ni wanasayansi Mohsen Fakhrizadeh anayeisaidia nchi hiyo kuwa na nishati ya nyuklia.

Kwa mujibu wa wizara hiyo ilibainisha kuwa Mohsen Fakhrizadeh, magaidi waliyojihami kwa silaha waliilenga gari lililokuwa limembeba mwanasayansi huyo, ambaye ndiye anayeongoza kitengo cha utafiti na uvumbuzi.

Taarifa ilieleza kuwa baada ya makabiliano kati ya magaidi hao na walinzi wa mwanasayansi huyo, hatimaye alijeruhiwa na kukimbizwa hospitali. “Kwa bahati mbaya jitihada za madaktari kuokoa maisha yake hazikufanikiwa na muda mfupi baadaye akafariki.”

Taarifa zilizotolewa baadae katika vyombo vya habari nchini Iran vilieleza kuwa gari alilopanda mwanasayansi huyo lilishambuliwa kwa risasi mfululizo na alijeruhiwa kwa risasi kadhaa mwilini.

Mauaji ya mwanasayansi huyo alitokea katika eneo la mji wa Ab-Sard uliopo mashariki mwa Tehran, ambapo mamlaka za eneo hilo zilithibitisha kifo chake masaa kadhaa na kusema baadhi ya washambuliaji pia waliuawa.

Fakhrizade, 63, alikuwa mwanachama wa kikosi cha walinzi wa kimapinduzi cha Iran na alikuwa mtaalamu wa uzalishaji wa makombora. Kulingana na shirika la habari la Fars, hii ndio sababu shirika la kijasusi la Israel kwa muda mrefu lilitaka kummaliza mwanasayansi huyo.

Shirika la habari la Fars awali liliripoti kuhusu mlipuko wa gari katika mji wa Absard, huku waliyoshuhudia tukio hilo wakdai kuwa watu watatu hadi wanne waliyodaiwa kuwa magaidi waliuawa.

Kama mkuu wa wizara ya ulinzi katika kitengo cha utafiti na uvumbuzi, Fakhrizadeh bila shaka alikuwa kiungo muhimu. Ndio maana waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alitoa onyo, miaka miwili iliyopita akimtaja kwa jina mwanasayansi huyo.

Tangu Iran ilipoanza kukiuka utekelezaji wa mktaba wa nyuklia uliyofikiwa mwaka 2015, nchi hiyo imeendelea mbele na hatua za kurutubisha madini ya urani kuimarisha uzalishaji huo kupita kiwango kilichokubaliwa.

Maofisa wa Iran wanasema mauaji hayo ni hatua za kuirejesha nyuma Iran, lakini utafiti na maendeleo ni vitaendelea nchini humo. “Hatuwezi kurudi nyuma,” Balozi wa zamani wa Iran katika Shirika la Kimataifa la Kawi ya Atomiki (IAEA), Ali Asghar Soltanieh.

Kwa upande wake, rais wa Iran Hassan Rouhani alisema mauaji ya mwanasayansi wake wa masuala ya nyuklia hayatalemaza mpango wa nyuklia wa nchi hiyo.

Ikiwa Mohsen Fakhrizadeh alikuwa kiungo muhimu kama vile Israel inavyodai, basi mauaji yake yanaashiria jaribio la kupunguza kasi ya Iran kuendelea mbele na mpango wake wa nyuklia.

Huku rais mteule wa Marekani, Joe Biden, akizungumzia mipango ya kurudisha Washington katika mkataba wa nyuklia wa Iran, mauaji ya mwanasayansi huyo huenda yalilenga kusambaratisha majadiliano yoyote ya siku zijazo kuhusu suala hilo.

Kufuatia mauaji hayo, waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Javad Zarif alisema kuna ushahidi unaoashiria uhusika wa Israel katika mauaji ya Mohsen Fakhrizade, lakini hakuweka wazi ni nani hasa aliyefanya shambulizi hilo.

Uthibitisho wa mauaji hayo unatolewa katikati ya wasiwasi mpya kuhusu kiwango cha urutubishaji wa madini ya urani ambayo taifa hilo inayazalisha.

Mnamo mwaka 2015, makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na mataifa makubwa yaliweka ukomo wa uzalishaji wa madini hayo ya urani, lakini rais Donald Trump alijiondoa miaka mitatu baadae.

Wakati huu rais mteule wa Marekani, Joe Biden ameahidi kuirejesha Marekani kwenye makubaliano hayo, ingawa wachambuzi wanasema atakabiliwa na changamoto kubwa kulifanikisha lengo hilo.

Msemaji wa shirika la nguvu za Atomiki la Iran, AEOI Behrus Kamalwandi alisababisha sintofahamu kwa kuzikana ripoti za kifo cha mwanasayansi huyo akisema “wanasayansi wetu wote wako salama”.

Hali hiyo ya sintofahamu iliibuka kwa kuwa Fakhrizadeh alikwishaondoka AEOI na amekuwa akifanya kazi kwenye idara ya utafiti na uendelezwaji wa teknolojia katika wizara ya mambo ya kigeni.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alietoa wito wa kujizuia baada ya mauaji hayo. Msemaji wa Umoja huo Farhan Haq aliliambia shirika la habari la DPA kwamba ” Tumezipata taarifa kwamba mwanasayansi wa nyuklia wa Iran ameuawa karibu na Tehran.

Mwanasanyansi huyo kwa muda mrefu amekuwa akichukuliwa na mataifa ya magharibi kama kiongozi wa programu ya siri ya bomu la nyuklia. Mauaji hayo huenda yakaibua mzozo mpya kati ya Iran na wapinzani wake, katika wiki za mwisho za utawala wa serikali ya rais Donald Trump wa Marekani.

Hassan Rouhani

Lakini pia kuleta ugumu katika juhudi zozote zinazotarajiwa kufanywa na Biden katika kufufua makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2018, yaliyofikiwa chini ya utawala wa Barack Obama.

Mshauri wa masuala ya kijeshi wa kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameapa kulipiza kisasi kikali kwa wauaji wa shahidi huyo. “Katika siku za mwisho za maisha ya kisiasa ya mshirika wao Trump, mazayuni wanataka kuongeza shinikizo dhidi ya Iran na kuanzisha vita kamili,” Hossein Dehgan aliandika kwenye twitter.

Israel imekataa kuzungumza chochote. Ikulu ya White House, wizara ya ulinzi, Pentagon na wizara ya mambo ya kigeni pamoja na shirika la kijasusi la Marekani, CIA pia yamekataa kutamka chochote kuhusu mauaji hayo, ikiwa ni pamoja na timu ya mpito ya rais mteule Joe Biden.

Fakhrizadeh alikuwa mwanasayansi pekee wa Iran aliyeitwa katika “tathmini ya mwisho” ya shirika la kimataifa la nguvu za atomiki ya 2015, ya maswali ya wazi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Ripoti hiyo ilisema alisimamia shughuli “zilizounga mkono mwelekeo wa kijeshi kwa mpango wa nyuklia wa Iran “.

Lakini pia alikuwa ni mtu muhimu wakati waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipokuwa akiwasilisha ripoti akiituhumu Iran kwa kuendelea kuzalisha silaha za nyuklia mnamo mwaka 2018.