RABAT, MOROCCO

VUGUVUGU la harakati ya Polisario imezishambulia ngome za Morocco katika eneo la Karkarat kusini mwa Sahaha Magharibi.

Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, mapigano yanaendelea kati ya Harakati ya Polisario na jeshi la Morocco zikiwa zimepita wiki mbli tangu kufunguliwa kivuko cha mpakani cha Karkarat kusini mwa Sahara Magharibi.

Jeshi la Morocco lilijenga matuta katika eneo la Karkarat kwa lengo la kurahisisha usafiri wa malori ya bidhaa yanayotumia kivuko cha mpaka wa Karkarat.

Safari za malori baina ya Morocco na Mauritania zilianza tena pamoja na kujengwa matuta hayo yaliyotajwa na Harakati ya Polisario kuwa ya fedheha.

Harakati ya Polisario iliitaja hatua hiyo ya Morocco kuwa ya kichokozi na ndio maana harakati hiyo ilitekeleza mashambulizi katika ngome za jeshi la nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa, Harakati ilieleza kuwa, wapiganaji wake walizishambulia ngome za jeshi la Morocco kwa silaha nzito na kuvisababishia hasara vikosi vamizi.

Harakati ya Polisario ni taasisi ya kisiasa na kijeshi inayoundwa na watu kutoka Sahara Magharibi huko kaskazini magharibi mwa Afrika na kusini mwa Morocco ambayo inaendesha mapambano kwa ajili ya uhuru wa eneo hilo.