NA HUSNA MOHAMMED

IKIWA dunia iko katika kuadhimisha kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia iliyoanza Novemba 25 na kukamilika Disemba 10 mwaka huu Zanzibar kama sehemu ya dunia ina mengi ya kutafakari kutokana na janga la ukatili wa kijinsia unaoendelea asiku hadi siku hapa visiwani.

Japo Kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Tupinge Ukatili wa Kijinsia:Mabadiliko Yanaanza na Mimi’ ni kaluli ambayo inabeba dhima ya kila siku jinsi ya kutafuta njia ya kuyapunguza seuze kuyamaliza majanga haya yanayowasubi wanawake na watoto katika jamii zetu kila uchao.

Nasema hivyo kwa kuwa ni nadra sana kusikiliza, kuangalia ama kusoma chombo chochote cha habari ambacho hutapata taatifa zinazohusiana na ukatili wa kijinsia.

Ingawa kauli mbiu hii inatoa wito kwa kila mmoja wetu kuchukua hatua dhidi ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia ambalo bado ni tatizo kubwa nchini Tanzania na duniani kwa ujumla.

Tafiti mbalimbali zinaonesha ukubwa wa tatizo mathalani ripoti ya utafiti wa Afya na Hali ya Watu Tanzania ya mwaka 2015-2016, inaonesha kuwa asilimia 40 ya wanawake na wasichana wenye umri kati ya miaka 15-49 wamepitia ukatili wa kimwili katika Maisha yao.

Kwa upande wa ukatili wa kingono, Ripoti ya Polisi juu ya makosa dhidi ya utu iliyotolewa mwaka 2019, imeonesha kuwa kati ya matukio 11,759 yaliyoripotiwa, mwaka 2018 matukio 7,617 yalikuwa ni makosa ya ubakaji ambayo ni sawa na asilimia 64.7.

Rushwa ya ngono, hususan katika vyuo vikuu imekuwa ni tatizo kubwa. Ripoti ya utafiti uliofanywa na Takukuru katika chou kikuu cha Dar es salaam na chuo kikuu cha Dodoma inaonesha zaidi ya asilimia 50 ya wahojiwa walieleza uwepo wa ngono katika vyuo vikuu.

Tafiti zinaoonesha kuwa vitendo hivyo vinafanywa na watu wanaofahamika na wahanga wakiwemo wapenzi, watu wa karibu, marafiki na watu wenye mamlaka.

Hivyo basi, kauli mbiu ya mwaka huu inamtaka kila mtu kuchukua hatua za kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia, kuhakikisha kuwa sauti za wahanga na wanaharakati zinasikika ili kukomesha vitendo vyote vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto.

Pamoja na mambo mengine, kampeni ya mwaka huu imeangazia katika maeneo matano ambayo ni ukatili majumbani, ubakaji, ndoa za utotoni, ukatili dhidi ya wenza (intimate partners violence) na rushwa ya ngono.

Katika kipindi hiki cha kampeni ya siku 16, za kupinga ukatili wa kijinsia kutakuwa na shughuli mbalimbali ambazo ni  pamoja na siku ya wahariri ambayo imeandaliwa ili kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari katika kuongeza uelewa wa maswala ya ukatili wa kijinsia, takwimu za ukatili na jinsi ya kuandaa ripoti za kesi za Ukatili wa Kijinsia.

Kutakuwa na siku ya kutoa Tuzo kwa mabalozi wa kupinga ukatili wa kijinsia, pia kutakua na midahalo mbali mbali juu ya maswala mtambuka yanayohusu ukatili wa kijinsia pamoja na shughuli nyingine zitakazoendelea kufanyika katika kipindi chote cha kampeni ndani ya siku zote kumi na sita 16 za kampeni.

Ili kuona vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia vinapungua ma kuondoka kabisa tunatoa wito kwa jamii, viongozi wa dini, taasisi na idara za serikali, asasi za kiraia, taasisi binafsi pamoja na wanahabari kupaza sauti, kuchukua nafasi katika kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Kwa mukhtadha huo basi kila mtu awe sehemu ya mabadiliko, kwa pamoja kupitia kauli mbiu ya mwaka huu.