NA TAKDIR ALI

WANANCHI wametakiwa kubadilika kwa kufanya usafi katika maeneo yao, ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya nane katika kuweka mazingira safi.

Diwani wa kuteuliwa Wilaya ya Magharibi ‘’B’’ Thuwaiba Jeni Pandu, ameyasema hayo huko Taveta na mbarali wakati alipofanya ziara ya kuangalia maeneo yanayotuama maji katika kipindi cha mvua.

Amesema Serikali imedhamiria kuweka usafi katika Jiji, Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri, ili kuwa kivutio cha wageni wanaoingia nchini na kupiga vita adui maradhi.

Aidha, amesema Serikali tayari imeshaweka Sheria ndogo ndogo, hivyo ni vyema Wananchi hao kutekeleza wajibu wa kudumisha usafi, ili kuepukana na adhabu zinazoweza kujitokeza.

Mbali na hayo, amewakumbusha Wazazi na Walezi kuwa Waangalifu kwa Watoto wao katika kipindi hiki cha mvua za vuli zinazoendelea kunyesha sambamba na kuepuka maradhi ya Mripuko ikiwemo kipindupindu na Matumbo ya kuharisha.

Nao Wakaazi wa Taveta na Mbarali Wilaya ya Magharibi ‘’B’’ wameliomba Baraza la Manispaa Wilaya ya Magharibi ‘’B’’ kuwawekea maeneo maalum ya kutupia taka, ili kuepuka kuzagaa ovyo kwa kutupwa maeneo yasio rasmi ikiwemo yanayopita Maji, ili kunusuru athari zinazoweza kujitokeza.