NA LAYLAT KHALFAN

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, amemuagiza Injinia wa Wizara hiyo, kuishughulikia haraka barabara ya Mwakaje hadi Mwachealale, kwa kiwango cha kifusi, ili kukidhi matakwa ya wananchi.

Alisema sijambo zuri kwa maeneo kama hayo kuwa hadi leo hawana njia sahihi ya kuendeleza shughuli zao huku ukizingatia wanahitaji kusafirishiwa bidhaa nyingi kutoka maeneo hayo kwa ajili ya kukuza soko lao na kipato kwa ujumla.

Alisema wananchi wa wanaoishi katika maeneo hayo wamekuwa wakipata tabu katika shughuli zao za kila siku hususan katika kipindi hichi cha mvua zinazoendelea kunyesha.

Wazir Masoud, alliyasema hayo wakati akitembelea barabara za ndani Wilaya ya Magharibi ‘A’ na kugundua kuwa barabara hiyo imekuwa ni kizingiti kikubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.

“Kutokana na usumbufu huu haraka iwezekanavyo barabara hii ijengwe ndani ya mwezi huu wa Disemba kwani bila kuharakisha gharama zake zitakuwa nyingi na wananchi wataendelea kuumia siku hadi siku’, alisema.

Aidha, alimsisitiza Injinia huyo kuhakikisha barabara hiyo inajengwa kwa kiwango kinachokubalika na kinachoendana na barababara hiyo na sio kuondoa njiani, kwani kufanya hivyo watakuwa wamefikia dhamira ya upatikanaji wa maendeleo ndani ya kijiji hicho.

Mkuu wa Injiani kutoka Wizara hiyo, Ali Omar Ali, alisema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 3.6, atahakikisha inakamilika mapema ifikapo Januari, ili kuwarahisishia huduma muhimu wakaazi wa eneo hilo.

Naye Mwakilishi wa jimbo la Mfenesini, Machano Othman, alisema Magharibi ‘A’ wanatatizo kubwa la barabara, hivyo hivyo alimshauri Waziri huyo, kuangalia uwezekano wa kujengewa barabara nyengine za ndani, ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wa eneo hilo.