Walioomba Uspika BLW wajadiliwa

NA ASYA HASSAN

KAMATI Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar imekutana jana kufanya mapendekezo ya wanachama wa chama walioomba kuteuliwa kuteuliwa kugombea nafasi ya Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Kikao hicho kiliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambae pia ni Rais mstaafu wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kilipitia maombi ya wanachama wa chama hicho waliojitokeza kuwania nafasi hiyo inayioshikiliwa na Zubeir Ali Maulid.

Akizungumza na gazeti hili Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCCM Zanzibar, Catherina Peter Nao, alisema katika siku mbili zilizowekwa kwa wanachama kuchukua na kurudisha fomu, wanachama watano akiwemo Spika Zubeir waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Aliwataja wanachama hao kuwa ni Yussuf Suleiman Khalfan, Mahamoud Mohammed Mussa, Tum Abdi Ali na Dk. Ameir Haidar Mshenga ambao majina yao yatajadiliwa na baadae kupendekezwa katika vikao vyengine vya chama kwa uteuzi.

Alisema kabla ya kikao cha kamati maalum, sekretarieti ilikutana kuandaa agenda za kikao hicho ambacho gazeti hili linakwenda mitamboni kikao hicho kilikuwa kinaendelea katika afisi kuu ya ccm Zanzibar, Kisiwandui.

Alifafanua kuwa chama hicho katazingatia mambo mbalimbali juu ya kumpata kiongozi huyo ikiwemo sifa ya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa baraza la wawakilishi na kuwataka wananchi na wanachama wa chama hicho kuendeleza kuitunza amani na utulivu.