NA MWANTANGA AME

MWENYEKITI wa Chama cha ADA TADEA, Juma Ali Khatibu, amewataka viongozi wa vyama vya upinzani kumuunga mkono Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ili aweze kutekeleza vizuri Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapiduzi aliyoinadi.

Khatibu, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya chama hicho na muelekeo wa serikali ya awamu ya nane, ofisini kwake Mombasa Kwa Mchina, Unguja.

Alisema chama chao kinaunga mkono hatua ya serikali iliyopo madarakani na uamuzi wa Rais kuweka wazi msimamo wake wa kuonesha ana dhamira ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Alisema hatua ya Dk. Mwinyi kuwapa maagizo 13 mawaziri wa serikali yake hadharani ni njia nzuri ya kuthibitisha uwazi na uwajibikaji anaouhitaji katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi zao.

“Ili mafanikio yaweze kufikiwa ni vyema kwa vyama vya upinzani vikaona umuhimu wa kudumisha amani na kuiunga mkono serikali iliyopo madarakani ili iweze kutekeleza ilani yake,” alisema Khatibu.

Kutokana na hilo Khatib, alisema kwa vile uchaguzi mkuu umemalizika, kinachotakiwa sasa jamii ishirikiane na serikali yao ili kuipa nafasi ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema hilo ni jambo la msingi kwa vile katika hotuba ya Rais aliyoitoa katika Baraza la Wawakilishi imebeba mambo mengi ikiwemo sekta muhimu kwa kukuza uchumi ikiwemo ya Utalii na Uchumi wa Buluu, jambo ambalo litaongeza kupatikana kwa ajira kwa vijana wa Zanzibar.

“Rais ameanza vizuri na nikiwa Mwenyekiti wa chama changu, tunamuunga mkono ametupa moyo lazima wananchi tumuunge mkono afanikishe ilani, lazima tubadilike ili tuweze kwenda sambamba na kasi yake tumeona dalili nzuri,” alisema.

Akizungumzia uteuzi wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, Khatibu alimpongeza na kueleza ana matumaini makubwa kutokana na utendaji wake katika nafasi mbali mbali ikiwemo ya Mkuu wa Mkoa Kusini, Pemba.

“Sina shaka na uteuzi wa mheshimiwa Hemed (Makamu wa Pili wa Rais) kwani ni mtu tuliyefanya kazi pamoja na kuiletea matunda serikali. Tunaahidi kumpa kila aina ya ushirikiano katika majukumu yake,” alisema Khatibu.

Akieleza uchapakazi wa makamu huyo wa rais, Khatib alieleza kuwa alipokuwa Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum katika serikali ya awamu ya saba, ilipoundwa kamati ya kufuatilia mashamba ya serikali, Hemed alichangia kubainika kwa upotevu wa shilingi Bilioni 3.5, jambo linaendelea kufanyiwa kazi.