NA MARYAM HASSAN

MKAAZI mmoja wa Donge wilaya ya Kaskazini ‘B’ mkoa wa Kaskazini Unguja, aliyeshitakiwa kwa kosa la kusababisha kifo cha Fahmi Othman Juma, ameiomba mahakama ya mkoa Vuga kumpatia dhamana.

Ombi hilo amelitoa mbele ya Hakimu Yesaya Kayange, mara tu baada ya kusomewa shitaka lake hilo ambalo alilikataa.

Mshitakiwa huyo ni Hassan Ali Mussa (29), ambaye alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na kosa la kusababisha kifo kutokana na uzembe.

Shitaka hilo alisomewa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Fatma Emmanuel.

Katika maelezo yake, Wakili huyo alidai kuwa, mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Februari 23 mwaka huu majira ya saa 4:00 za asubuhi, huko Mfenesini wilaya ya Magharibi ‘A’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alidaiwa kuwa, siku hiyo mshitakiwa huyo akiwa anaendesha gari aina ya NOAH yenye nambari za usajili Z 936 GA, akitokea upande wa Mfenesini kuelekea maeneo ya kwa Nyanya, bila ya hadhari na kwa uzembe alimgonga mtoto wa miaka mitano na kusababisha kifo chake.

Mahakama ilifahamishwa kuwa, mtoto huyo alikuwa akitembea kwa miguu na kuvuka barabara, jambo ambalo ni kosa kishera.

Mara baada ya kusomewa shitaka lake hilo, mshitakiwa huyo alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana jambo ambalo limekubaliwa.

Kufuatia ombi hilo, Hakimu Kayange alimtaka mshitakiwa kusaini bondi ya shilingi 2,000,000 pamoja na kudhaminiwa na mdhamini mmoja ambae alitakiwa kusaini kima hicho hicho cha fedha kwa maandishi.

Pamoja na masharti hayo, mdhamini huyo alitakiwa kuwasilisha barua ya Sheha wa Shehia anayoishi sambamba na kopi ya kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.