NA ABOUD MAHMOUD

TIMU ya soka ya Azam FC inayoshiriki ligi kuu Tanzania Bara imerudisha tena utaratibu wa kutoa tuzo za mwezi kwa mchezaji bora.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Habari wa timu hiyo,Thabit Zakaria ‘Zaka’ wakati alipokua akizungumza na Zanzibar Leo kwa njia ya simu akiwa jijini Dar es Salaam.

Zaka alisema timu hiyo imeamua kurudisha tuzo hizo ambazo zitaanza kutolewa Novemba 5 mwaka huu kwa mchezaji bora wa mwezi Septemba na Oktoba.

“Tunatarajia kuanza kutoa tuzo hizi tarehe 5 ya mwezi huu ambapo siku hiyo tutakua tunacheza na Dodoma FC kwenye mchezo wa ligi kuu, ambapo siku hiyo tutatoa tuzo mbili kwa mchezaji wa Septemba na Oktoba,”alisema Zaka.

Ofisa huyo alisema tuzo hizo zinapatikana baada ya mashabiki kumpigia kura mchezaji .

Zaka aliwataja wachezaji ambao wameingia katika kinyang’anyiro hicho kwa mwezi wa Septemba ni Prince Dube,Abdullah Kheri ‘Sebo’, David Mapigano ‘Kisu’, Bruce Kangwa na Salum Abubakar ‘Sure boy’.

Aidha aliwataja wachezaji walioingia kwa mwezi wa Oktoba ni pamoja na Prince Dube, Ali Niyonzima, Obley Chora Chilwa, Salum Abubakar ‘Sure boy’, na Bruce Kangwa.

Ofisa huyo alifahamisha kuwa upigaji wa kura utakaotumika ni wa njia ya ujumbe mfupi wa maneno kwa njia ya simu utakaotumwa na shabiki kwa kuandika jina la mchezaji anaemtaka pamoja na mwezi .

“Mashabiki wa Azam watatakiwa kumchagua mchezaji anaestahili kupewa tuzo hiyo kwa kutumia nambari ya simu 0743 408926 ambayo wataitumia kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno ambapo wataandika jina la mchezaji pamoja na mwezi anaotaka apate tuzo hiyo,”alieleza.