VISIWA wa Barbados vinapatikana mashariki ya eneo la karibian, ambapo visiwa hivyo vilikuwa chini ya utawala wa Uingereza ambapo malkia wa Elizabeth II ndiye mkuu wa taifa hilo.

Ni visiwa maarufu katika eneo la Caribbean, ambapo lilijipatia uhuru wake kutoka kwa Uingereza mnamo mwaka mwaka 1966, hata hivyo, malkia huyo ameendelea kuwa mtawala kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.

Barbados ni nchi inayojitegemea sana katika uchumi utokanao na shughuli za uzalishaji na usafirishaji wa sukari, pia utalii una sehemu kubwa sana katika uchumi wa taifa hilo.

Unaweza usiamini, lakini katiba takriban za nchi 15 hapa duniani zinatambua malkia Elizabeth II kuwa ni mkuu wa nchi hizo, huku zikiongozwa na serikali za kidemokrasia zinazofanya uchaguzi.

Nchi nyengine ambazo katika zao zinamtambua malkia kuwa ndiye mtawala  ni pamoja na Australia, Canada, New Zealand, Jamaica na visiwa kadhaa vilivyopo katika eneo la Caribbean na bahari ya hindi.

Waziri mkuu wa sasa wa Barbados ni Mia Mottley, alichaguliwa mwaka 2018, ambapo ameweka histoa kuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo katika visiwa hivyo.

Mtawala wa kisiwa hicho, malkia Elizabeth ll alifanya ziara kuitembela ardhi ya Barbados ambayo ni sehemu ya utawala wake mnamo mwaka 1977, ambapo alipokelewa kwa shangwe kubwa.

Hata hivyo kwa muda mrefu sasa wanasiasa na wananchi wa Barbados, wana mawazo ya kutaka nchi yao iwe taifa huru (Jamhuri) na iache kuongozwa ama kupokea miongozo au sera kutoka London.

Kutokana na hali hiyo wanasiasa nchini humo tayari wametangaza ni ya ya kumuondoa malkia wa Uingereza Elizabeth II kama kiongozi mkuu wa wa nchi hiyo na kuwa Jamuhuri kamili.

Hivi karibuni waziri mkuu wa visiwa hivyo, Mia Mottley alitoa kauli ya wazi ambapo alisema, “Muda umewadia wa kuachana na historia yetu ya kikoloni”. Akimaanisha sasa wanataka nchi hiyo iwe Jamhuri kamili.

Kauli hiyo ina lengo la kumaliza mchakato huo wakati wa kumbukumbu ya miaka 55 ya uhuru wake kutoka Uingereza, itakayofanyika mwezi Novemba mwaka 2021.

Kasri la Buckingham la matawala wa Uingereza malkia Elizabeth II, lilijibu kauli hiyo ya waziri mkuu Barbados kwa kueleza kuwa ni suala la serikali na watu wa visiwa vya Barbados kuamua majaliwa yao.

Chanzo cha habari katika kasri la Buckingham kimesema kuwa wazo hilo halikuja tu ghafla na limekuwa likizungumzwa hadharani mara nyingi na wanasiasa nchini Barbados.

Kauli hiyo ilikuwa sehemu ya taarifa ya serikali ya kifalme, ambayo imetanabaisha sera za serikali na programu katika kuelekea vikao vipya vya bunge. Wakati ikisomwa na gavana mkuu, ina maana kuwa imeandikwa na waziri mkuu wa nchi.

Hotuba hiyo pia ilinukuu onyo kutoka kwa Errol Barrow, waziri Mkuu wa kwanza wa Barbados baada ya kupata uhuru, ambaye alisema kwamba nchi hiyo haipaswi kurandaranda kwenye maeneo ya majengo ya wakoloni.

Sio sauti yake tu huko Barbados ambayo imekuwa ikipendekeza kuhama kutoka kwenye utawala wa kifalme. Tume ya ukaguzi wa katiba ilipendekeza hadhi ya jamhuri kwa Barbados mnamo 1998.

Mtangulizi wa waziri mkuu wa sasa, Freundel Stuart, pia alitetea kuhama kutoka kwa mfumo wa utawala wa kifalme kwenda kwa serikali ya Jamhuri katika siku za usoni.

Barbados haitakuwa koloni la kwanza la Uingereza katika Carribean kuwa jamhuri, kwani nchini ya Guyana nayo ilichukua hatua hiyo mnamo mwaka 1970, chini ya miaka minne baada ya kupata uhuru kutoka kwa Uingereza.

MALKIA Elizabeth II wa Uingereza (kushoto) akisalimiana na gavana mkuu wa Barbados, Sandra Mason wakati gavana huyo alipofanya ziara katika kasri la malkia Buckingham mnamo mwaka 2018.

Nchi nyengine katika eneo la Caribbean zilizochukua hatua ya kuwa Jamhuri ni pamoja na visiwa vya Trinidad na Tobago ambao walifanya hivyo mnamo mwaka 1976 na Dominica mnamo mwaka 1978.

Nchi zote tatu zilizochukua hatua hiyo, zimekuwa ndani ya Jumuiya ya Madola, umoja wa nchi huru za makoloni ya zamani ya Uingereza pamoja na nchi nyingine ambazo hazina mafungamano ya kihistoria na Uingereza.

Kwa hakika ni jambo lisilo la kawaida kwa nchi kumuondoa malkia kama kiongozi wao, ambapo nchi ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa Mauritius mwaka 1992.

Nchi 15 ambazo ni sehemu ya dola ya malkia zinaonekana kuthamini mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizo na Uingereza.

Ni kweli, baadhi wamekuwa wakiongelea suala ya kuwa na wakuu wao wa nchi na kuachana na utawala wa kifalme, lakini mara nyingi malengo ya kisiasa yamekuwa kikwazo.

Si mara moja kwa wanasiasa wa Barbados kueleza nia yao ya kuwa Jamuhuri, hata hivyo suali ni kuwa kama uamuzi huu utalingana na nchi nyengine zilizokwisha chukua hatua hiyo.

Umuhimu wa kumuondoa malkia kuwa mtawala katika nchi ya Barbados ni kutaka kuondokana na historia ya kikoloni.

Katika dhana ya kampeni ya Black Lives Matter, itakuwa jambo linalosubiriwa kuona kama hatua hii italeta msukumo wa kisiasa kwa serikali za Caribbean kuchukua mkono huo huo.

Na ikiwa hili litatokea, na kuondolewa kwa malkia kama mkuu wa nchi kutalingana na, tuseme, kuondolewa kwa sanamu ya mfanyabiashara wa watumwa, basi hiyo inaweza kusababisha maswali magumu kwa familia ya kifalme ya Uingereza na Jumuiya ya Madola.