NA MWANAJUMA MMANGA

HALI ya biashara katika soko la Mwanakwerekwe imeanza kuimarika baada ya kudorora siku chache kabla ya uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, Mkuu wa soko hilo Omar Kilian Othman, alisema hali ya biashara ilianza kushuka katika wiki ya mwisho kuelekea uchaguzi na baadhi ya bidhaa kuadimika kutokan.

Alizitaja baadhi ya bidhaa hizo kuwa ni pamoja na zinazoingia nchini kutoka Tanzania bara kama vile tungule, mbatata, keroti, vitunguu maji, vitunguu thomu, pilipili boga na nazi.

Alisema hali hiyo ilipelekea kupanda bei kwa bidhaa hizo ikilinganishwa na kipindi cha mwezi wa Septemba mwanzoni huku watu wengi wakionenekana kununua bidhaa kwa wingi.

“Katika kipindi hicho, baadhi ya bidhaa zilipanda bei na kufikia kilo shilingi 1,500 kwa Tungule ambapo awali ilikuwa shilingi 1,200 wakati mbatata ilifika kuuzwa kilo shilingi 1,200 ambapo awali ilikuwa shilingi 700,” alisema Omar.

Aliongeza kuwa vitunguu maji wakati wa kipindi cha uchaguzi uchaguzi vilikuwa shilingi 2,000 kwa kilo kinyume na shilingi 700 za awali lakini hivi sasa vinauzwa 1,000, huku bei ya nazi ambayo kabla ya kipindi cha uchaguzi ilikuwa ikiuzwa shilingi 700 ilipanda bei mara mbili ya ilivyokuwa awali ingawa kwa sasa inauzwa shilingi 1,000.

Aidha Omar alisema bei ya keroti ambayo awali ilikuwa ikiuzwa shilingi 900, ilifika shilingi 2,000 katika kipindi hicho na hivi sasa inauzwa shilingi 1,500 kwa kilo huku bei ya vitunguu thomu kilo moja ilifika shilingi 7,500 ambapo hapo awali ilikuwa shilingi 5,000 kama ilivyo sasa.

Kwa upande wa vitoweo, Omar alisema katika kipindi hicho bei ya nyama safi ya ng’ombe iliuzwa kwa shilingi 1,2000, nyama mchanganyiko ilikuwa shilingi 8,000 ambapo wakati bei ya awali  ilikuwa shilingi 10,000 kwa nyama safi na shilingi 8,000 kwa nyama mchanganyiko.

“Kuna baadhi ya bidhaa zilipanda kutokana na kuzuliwa kwa usafiri wa majahazi ambayo ndio hutumika Zaidi kuleta bidhaa hizo Zanzibar na kupelekea bei kuwa juu,” alieleza mkuu huyo wa soko.

Alisema kwa upande wa nafaka na bidhaa nyengine za chakula kutoka Tanzania bara zilisita kuja Zanzibar hususani mchele ulipungua sokoni hapo huku bidhaa zinazolishwa nchini zilikuwa zinaingia sokoni kama kawaida.

Mbali ya sababu za usafiri, Omar alieleza kuwa kuanzia Oktoba 25 hadi 30 wafanyabiashara wengi wa soko hilo walifunga biashara zao kutokana na kushiriki katika kampeni lakini pia hofu ya usalama wao na mali zao.