WASHINGTON,MAREKANI

RAIS  mteule wa Marekani Joe Biden amechukua hatua za kwanza kuelekea Ikulu katika siku 73, wakati Donald Trump kwa mara nyengine akikataa kukubali kushindwa na kujaribu kutilia shaka matokeo ya uchaguzi.

Huku salamu za pongezi zikimiminika kutoka kwa viongozi wa ulimwengu na wafuasi wakiendelea kusherehekea, Biden na makamu wa rais mteule Kamala Haris walizindua tovuti ya utaratibu wa mpito, ya BuildBackBetter.com pamoja na akaunti ya Twitter ya @Transition46.

Tovuti hiyo ina vipaumbele vinne ikiwa ni Covid-19, kuufufua uchumi, usawa wa rangi na mabadiliko ya tabia nchi.

Trump anapanga kuwasilisha msururu wa kesi mahakamani katika wiki ijayo kwa mujibu wa wakili wake Rudy Giuliani, ambaye alisema ana ushahidi mwingi wa kuwepo udanganyifu.

Rais wa zamani Goerge W. Bush alisema matokeo ni ya wazi na akaongeza kuwa alimpigia simu Rais mteule Biden na Harris kuwapongeza.