LILONGWE, MALAWI

RAIS wa Malawi ameagiza bodi ya mitihani ya kitaifa nchini humo kuvunjwa baada ya mitihani ya kitaifa ya mwaka huu kuvuja na kusambaa kwa mitandao ya kijamii kabla ya watahiniwa kuifanya.

Hatua ya mitihani hiyo kuvuja, ilipelekea mitihani ya kitaifa kuahirishwa na kupelekea wanafunzi kuingia mitaani kwa maandamano, wakikabiliwa na polisi waliowatawanya kwa kutumia gesi ya kutoa machozi.

Akihutubia taifa, Rais Lazarus Chakwera alisema kwamba wasimamizi wa bodi ya mitihani nchini humo wanastahili kufutwa kazi kwa kuzembea kazini na kupelekea mitihani ya kitaifa kuvuja.

Agizo hilo lina lilitolewa siku moja baada ya wizara ya elimu kufuta mtihani wa kitaifa kwa watahiniwa wa skuli za sekondari, uliokuwa umepangiwa kuanza Oktoba 27.

Rais Chakwera alisema kwamba hatua ya mitihani hiyo kuvuja ni dhihirisho kwamba bodi inayosimamia mitihani ya kitaifa haina uwezo wa kusimamia mitihani nchini humo.

Polisi walikamata wanafunzi 38 na walimu watatu kutoka skuli baada ya kupatikana na karatasi sita za mitihani zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Mkurugenzi wa bodi ya mitihani nchini Malawi Gerald Chiunda, aliwaambia waandishi wa habari kwamba huenda karatasi za mitihani zilivuja kutoka ofisini kwake na kwamba uchunguzi unaendelea.

Rais Chakwera aliamuru waziri wa elimu kuwaadhibu wahusika wote kabla ya mwezi huu wa Novemba kukamilika.