SANTIAGO DE CHILE,CHILE

MAELFU ya raia wameandamana kwenye mji mkuu wa Chile, Santiago, wakimtaka Rais Sebastian Pinera ajiuzulu kutokana na ukandamizaji wa polisi dhidi ya waandamanaji wenzao.

Polisi walitumia gesi ya machozi na maji yanayowasha kuwazuwia waandamanaji wapatao 500 kulifikia kasri la rais la Moneda.

Waandamanaji wengine walilizingira eneo mashuhuri la Alameda karibu na kasri hilo kwa takribani masaa mawili.

Maandamano hayo yalifanyika ikiwa ni wiki tatu tu tangu raia kupiga kura ya maoni ambayo iliipitisha kwa wingi katiba mpya kuchukuwa nafasi ya ile iliyorithiwa kutoka utawala wa kidikteta wa mwaka 1973 hadi 1990 wa Jenerali Augusto Pinochet.

Kura hiyo ya maoni ilikuwa ndilo dai la kimsingi baada ya miezi kadhaa ya maandamano ya umma yaliyoanza tangu mwezi Oktoba mwaka jana, ambayo awali yalikuwa dhidi ya kupanda kwa bei za usafiri wa umma, lakini kisha yakatanuka kuwakilisha hasira ya umma dhidi ya ukosefu wa usawa.