NA MWANDISHI WETU, PEMBA

MAHAKAMA ya mwanzo Chake Chake, imeiahirisha kesi ya tuhuma ya ubakaji inayomkabili aliyekuwa bosi wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC) wilaya ya Mkoani, baada ya Hakimu husika kutokuwepo mahakamani.

Kesi hiyo ambayo kwa sasa iko hatua ya kusikiliza mashahidi wa upande wa mashtaka, ililazimika kutua mahakama ya wilaya, baada ya Hakimu wa mahakama ya mkoa Chake Chake anaeindesha kesi hiyo kuwepo nje kikazi.

Hakimu wa mahakama ya mwanzo Ussi Mjengo, alisema Hakimu anaehusika na shauri hilo Abdull-razak Abdull-kadiri Ali yupo nje ya mahakama kikazi.

“Inabidi mtuhumiwa kesi yako tuiahirishe hadi Novemba 24, mwaka huu, maana Hakimu husika amepata dharura hivyo, mahakama hii haina uwezo wa kuendelea na shauri hili,’’alisema.

Awali Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Asia Ibrhamin, aliiambia mahakama hiyo, kuwa shauri hilo lipo kwa ajili ya kusikiliza mashahidi.

‘Shauri hili lipo kwa ajili kusikiliza mashahidi wa upande wetu, lakini kwa vile Hakimu hasika hayupo, naiomba mahakama hiyo kuliahirisha na kulipangia tarehe nyingine,’’alidai.

Ombi hilo halikupingwa na mahakamani hapo na Hakimu Ussi kuamua kuliahirisha hadi Novemba 24 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.