NA SAIDA ISSA, DODOMA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kesho anatarajiwa kulizindua bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hatua hiyo inakuja kufuatia wabunge wateule kuapa kwa siku mbili Jumanne na Jumatano ambapo zoezi hilo liliongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Akizungumza jana bungeni Ndugai alisema kesho Dk. Magufuli anatarajiwa kulihutubia Bunge kwa maana ya kuweka dira ya serikali pamoja na utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.

“Waheshimiwa Wabunge kabla hatujaendelea, niwaarifu kwamba kwenye mkutano wa kwanza wa Bunge jipya kama huu wa kwetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anahutubia Bunge kwa maana ya kuweka dira ya serikali yake kwa miaka mitano inayokuja na utekelezaji wa ilani ya chama kadri anavyoona inafaa,” alisema.

Alisema hutuba hiyo ni muhimu hivyo wabunge hao wanatakiwa kuwahi kufika ukumbini ili waweze kumsikiliza kwa umakini Rais.

Alisema siku hiyo katika viwanja vya Bunge kutakua na shughuli mbalimbali ikiwemo gwaride la kumpokea Rais pamoja na kuwapokea wageni mbalimbali.

Alitoa wito kwa wabunge ambao wameondoka Dodoma warudi mara moja kwa ajili ya zoezi hilo na wale ambao wanafikiria kuondoka wabaki ili kumalizia zoezi hilo.

“Na ni vizuri kila mmoja wetu akawepo na mbunge yeyote ambaye ametoka kwenda popote nitoe wito turudi Dodoma tayari kuisikiliza hotuba, tumpokee Rais wetu na tumpe kila aina ya ushirikiano, na wale mliokuwa mkifikiria   kuondoka msiondoke kwanza ili zoezi hilo liweze kwenda kwa salama na amani,” alisema

Jana asubuhi Spika wa Bunge alimaliza zoezi la kuwaapisha wabunge wote, wakiwemo mbunge wa CHADEMA jimbo la Nkasi Kaskazini, Aida Khenani naye aliapa pamoja na Mbunge wa Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Mtwara vijijijini, Shamsia Mtamba.

Wabunge wa Viti Maalum 19 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wao hawakuonekana wakati wa zoezi hilo la uapishaji.