Hotuba yake kutoa muelekeo wa Z’bar

Wananchi wasubiri kwa hamu kuisikiliza

NA LAILA KEIS

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi leo anatarajia kuzindua mkutano wa kwanza wa baraza la 10 la Wawakilishi, huko katika jengo la Baraza hilo Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Katibu wa Baraza hilo Raya Issa Msellem alisema, baraza hilo litazinduliwa majira ya saa 8:00 mchana, ambapo Rais Mwinyi atahutubia wananchi wa Zanzibar.

Alisema mbali na shughuli hiyo pia kutakuwa na mambo mengine mbali mbali ikiwemo uchaguzi wa Spika atakayeliongoza baraza hilo pamoja na kula kiapo cha uaminifu.

Shughuli nyengine itakayofanyika kabla ya kuzinduliwa kwa baraza ni kiapo cha uaminifu kwa wajumbe wote wa baraza hilo, uchaguzi wa naibu Spika na shughuli nyengine zitakazojitokeza.

Raya alibainisha kuwa hadi sasa wawakilishi wanaotarajiwa kuwepo katika baraza hilo ni kutoka Chama cha Mapinduzi na Chama cha ACT Wazalendo, ambao walishinda katika majimbo mbalimbali ya Zanzibar pamoja na viti maalum.

Aidha alisema matarajio ya baraza ni kuwa na mashirikiano ya pamoja katika kudumisha demokrasia kwa vyama hivyo ambayo itawajengea uwezo wananchi kushiriki katika shughuli za kuleta maendeleo ya nchi.

Sambamba na hilo aliwataka waandishi wa vyombo mbali mbali vya habari waendelee kutoa ushirikiano wa karibu katika kutoa taarifa za mikutano itakayoendeshwa kwenye Baraza hilo.

Katibu huyo alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kumaliza vyema zoezi la uchaguzi mkuu lililofanikisha kupata viongozi wapya watakaodumu madarakani kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wananchi walisema kuna umuhimu mkubwa wa kusikilizwa hotuba ya Rais ya ufunguzi wa Baraza la Wawakilishi kwani kawaida ndiyo inayotoa muelekeo wa nchi katika kipindi cha miaka mitano.

“Hotuba ya Rais ya ufunguzi wa Baraza la Wawakilishi ina umuhimu mkubwa kwani ndiyo dira ya nchi inakoelekea, hubainisha mipango na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na vipi atawasaidia wananchi”, alisema Mohammed Ali Ameir mkaazi wa Kwahani.

Naye Kombo Amour Haji (70), mkaazi wa Mikunguni mjini Zanzibar aliwaomba wananchi waisikilize kwa makini hotuba hiyo ambayo itaweka wazi mipango ya uendeshaji wa nchi.

“Kwa umri wangu mimi nishakuwa mzee katika kampeni zake Dk. Mwinyi aliahidi mambo mengi ikiwemo kujali wazee, najua katika hotuba yake ya leo suala hili litakuwemo”, alisema.