NA IS-HAKA OMAR

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka viongozi na wanachama wa chama hicho kuhakikisha wanaendeleza umoja hali ambayo itawawezesha kulinda maslahi ya chama hicho.

Dk. Shein ambaye pia ni rais mstaafu wa Zanzibar, alieleza hayo jana wakati akifungua kikao cha kawaida cha kamati maalum ya halmashauri kuu ya CCM Taifa Zanzibar, kilichofanyika ofisi za chama hicho zilizopo Kisiwandui.

Alisema pamoja na ushindi mkubwa uliopata chama hicho katika uchaguzi mkuu uliomalika hivi karibuni, wanachama na viongozi wa CCM lazima wadumishe umoja ambao utakiwezesha chama hicho kuwa imara zaidi.

Pamoja na mambo mengine kikao hicho kilipokea na kujadili mapendekezo ya wanaCCM walioomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Katika hatua ya kuwania nafasi hiyo wanaCCM wawili walijitokeza kuchukua na kurejesha fomu ya kugombea kuteuliwa nafasi ya Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi ambao ni Mgeni Hassan Juma na Mwanaasha Khamis Juma.

Kikao cha kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika Novemba 5 mwaka huu mjini Dodoma kiliamua kukasimu kwa kamati maalum kufanya uteuzi wa mwisho kwa wana CCM wanaoomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi.

Akizungumza katika kikao hicho Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema ataendelea kuwatumikia wananchi kwa uadilifu kama alivyoahidi katika kampeni.

Dk. Hussein, aliwasihi wajumbe wa kikao hicho kumshauri na kutoa maoni yao juu ya utendaji wake ili aende sambamba na kasi ya maendeleo nchini.

Naye mjumbe wa kamati kuu ya CCM ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah, aliwashukuru wananchi kwa uamuzi wao wa kuwachagua viongozi wa CCM kwa kura nyingi.

Pamoja na hayo alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi kwa kumuamini na kumteua ili amsaidie majukumu ya kiutendaji kupitia nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

”Nami naungana na msimamo wa rais wetu Dk. Hussein kuwa tumeaminiwa na wananchi na kutupa ridhaa, hivyo kama viongozi lazima tuwajibike kuwatumikia wananchi kwa vitendo ili wanufaike na rasilimali za nchi”, alisema Hemed.

Sambamba na hayo alisema kumalizika kwa uchaguzi wa mwaka huu ni matayarisho ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Kikao hicho cha kawaida kimefanyika kwa mujibu wa Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2017 ibara ya 109 (1), (3),(6) (a) -(d).