ADDIS ABABA,ETHIOPIA

WAZIRI Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ambaye pia ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ya mwaka 2019, ameliagiza jeshi la nchi hiyo kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya vikosi vya kabila dogo katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo la Tigray.


Serikali ya Ethiopia ilianza operesheni za kijeshi na ilidai kuwa vikosi vinyavyoiunga mkono serikali ya eneo la kabila la Tigray vilishambulia kambi ya jeshi siku iliyotangulia.
Serikali kuu ilitangaza hali ya dharura katika eneo la kaskazini ambako huduma ya simu na intaneti zilisitishwa.


Shirika la habari la Reuters lilimnukuu shuhuda mmoja akisema kuwa mashambulizi makali ya mizinga yalisikika katika eneo la Tigray, na kuwa wanajeshi takriban 24 walijeruhiwa na kutibiwa katika zahanati moja.
Abiy anayetoka kabila kubwa nchini humo la Oromo, alichukua wadhifa wa waziri mkuu wa nchi hiyo miaka miwili iliyopita. Kabla ya hapo, kabila dogo la Tigray lilishikilia sehemu kubwa ya madaraka ya kisiasa.


Abiy alishinda tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019 kwa kumaliza mzozo na nchi jirani ya Eritrea uliodumu kwa muda mrefu na kwa kuhamasisha demokrasia nchini mwake.
Lakini harakati za kidemokrasia zilisababisha kuongezeka kwa madai kutoka kwa makundi mbalimbali ya kikabila katika nchi hiyo yenye makabila mengi.