ZASPOTI
ASAMOAH Gyan, amesema, kurudi kwake Ghana na kusaini klabu ya Legon Cities haimaanishi kuwa anapanga kustaafu.
Nahodha huyo wa zamani wa Black Stars alisainiwa na klabu yake mpya kama mchezaji huru baada ya kukaa nchini India kumalizika mapema mwaka huu.


“Mtu anaweza kusema yuko karibu kustaafu au kitu chengine “, lakini, sisikii hilo na ninazingatia tu kazi yangu ya uchezaji na ndipo nitakapoona kitakachotokea”, aliiambia, BBC Sport Africa.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34, ambaye amesaini mkataba mpya wa mwaka mmoja ambao unaweza kudumu kwa miaka minne, alikataa kuondoa uwezekano mwengine wa kucheza nje ya nchi au kulazimisha kurejea kwenye timu ya taifa.


Mechi yake ya mwisho kwa Ghana ilikuwa kama mbadala kwenye mechi ya kipigo mbele ya Tunisia katika Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 nchini Misri.
“Inategemea jinsi kila kitu kinavyokwenda. Mimi ni mchezaji mpya na Legon Cities na lazima nizingatie mchezo wangu,” alisema, alipokua akijibu ikiwa mpango huo ni hatua ya muda mfupi.
“Hivi sasa ninahitaji kujiweka sawa na kuanza kufunga mabao na ndipo tutaona ni wapi hatma yangu iko na timu ya taifa. Vijana wanafanya vizuri, ni kizazi kipya hivi sasa na pia ninaangazia mambo yangu binafsi na soka yangu”.


“Lazima nifanye vizuri kwenye ligi kwanza, na hilo ndiyo jambo muhimu kwangu. Lazima nianze kucheza na kufurahia mpira wangu na itatokea kawaida ikiwa inakusudiwa kuwa. Kila kitu kinategemea mimi.”
“Wakati mwengine watu husahau kuwa ligi ya Ghana pia ni ligi ya kitaalamu”, alisema.
“Nilipata ofa na kila kitu kilikuwa sawa, kama mtaalamu lazima utathmini kila kitu. Ninajivunia kuwa kwenye ligi ya Ghana.


“Jambo muhimu zaidi ni kwamba walikuwa wazito juu ya mkataba. Mimi ni mtu makini, licha ya watu kuniona kama mtu wa kuchekesha pia, lakini, linapokuja suala la kufanya kazi, ni kazi. Kila kitu kinahusu uzito.
“Nipo Ghana na nipo nyumbani. Nimesaini klabu hii kwa sababu wana mradi mkubwa, wanataka kubadilisha mpira wa miguu wa Ghana. Nilikuja hapa kwa sababu, kwa hivyo wakati ninafurahia mpira wa miguu, pia tunafanya vitu nyuma ya pazia kwa manufaa ya Ghana.


Gyan, mfungaji bora katika historia ya Black Stars akiwa na magoli 51, alithibitisha kuwa ukocha ni kitu ambacho anatarajia kukifanya atakapostaafu.
Mara ya mwisho kwa Gyan kuchezea klabu za Ghana ilikuwa mwaka 2003, wakati alipoondoka Liberty Professionals na kujiunga na Udinese ya Italia.(Goal).