NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla amewataka watumishi wa umma kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu yao waliyopewa kwa kuhakikisha wanawatumikia wananchi.

Makamu huyo alieleza hayo jana muda mfupi baada ya kupokewa kwenye ofisi yake mpya akiwa kama mtendaji mkuu wa serikali wakati akizungumza na viongozi wa idara na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar hapo Vuga mjini Zanzibar.

Alisema baadhi ya viongozi ama watendaji watakaojihisi kwamba hawaendani na kasi ya serikali mpya ni vyema wakaondoka kwa heshima kabla ya kusubiri kulazimishwa kuondoka kwa kushindwa kuwajibika.

Alisema haipendezi kuona baadhi ya viongozi wa taasisi na wakuu wa vitengo wanafikiria maslahi binafsi hasa kwenye fursa za masomo, safari za nje ya Zanzibar bila ya kujali wafanyakazi wa chini.

“Haipendezi na haitawezekana kuona viongozi waandamizi na wakuu wa taasisi wanajipatia maposho ya safari na wasindwe kuwapatia haki zao wafanyakazi wao wa ngazi ya chini”, alisema.

Alitanabahisha kwamba akiwa mtendaji mkuu wa shughuli za serikali hatakuwa tayari kumbeba kiongozi au mtumishi yeyote aliyepewa dhamana na akashindwa kuitekeleza katika eneo lake la kazi.

Alionya kwamba akimgundua kiongozi anayetumia vibaya rasilmali za umma aelewe kwamba atakwenda na maji kwani atamchukulia hatua za kinidhamu mara moja.

Aliwataka watendaji hao wajisafishe kwa vile wao ndio wanaosimamia utendaji wa serikali na kuacha malalamiko yasiyo na msingi kwani pale vinapojitokeza vikwazo katika uwajibikaji wao taratibu ziko wazi za kuwasilisha changamoto zao zinazowakabili katika ngazi ya juu.

Hemed aliwashukuru viongozi wakuu waliostaafu wa serikali ya awamu ya saba Dk. Ali Mohamed Sheni na Balozi Seif Ali Iddi kwa ulezi wao mwema uliopelekea kuwajengea daraja ya pale walipofikia Viongozi wapya.

Aliwaomba viongozi hao wastaafu waendelee kuacha milango wazi kwa viongozi wapya ili pale watakapohitaji mawazo na busara zao katika uwajibikaji wa utumishi wa umma waweze kuitumia fursa hiyo adhimu.