Ateuliwa baada ya kuapa kuwa mjumbe wa baraza la wawakilishi, wengi wapongeza

NA MWANDISHI WETU

HATIMAE kitendawili cha nani atakuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kimeteguliwa jana baada rais wa zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kumteua Hemed Suleiman Abdulla kushika wadhifa huo.

Tangazo la uteuzi wa hemed ambae pia ni mkuu wa mkoa wa kusini unguja, lilitolewa na spika wa baraza la wawakilishi Zubeir Ali Maulid kabla ya kuakhirisha kikao cha kwa nza cha mkutano wa kwanza wa baraza la 10 lililoanza jana.

Aidha tangazo hilo lilifuatiwa na taarifa iliyotolewa na katibu wa baraza la mapinduzi na katibu mkuu kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliesema uamuzi huo unatokana na uwezo aliopewa Rais na katiba ya Zanzibar ambapo uteuzi huo ulianza Novemba 8 mwaka huu.

“Kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu namba 39(1) na 39(2) cha katiba ya Zanzibar yam waka 1984, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amemteua Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla kuwa makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Wakati Spika zubeir akisoma tangazo la uteuzi huo, wajumbe wa baraza hilo ambao awali walikula kiapo cha uaminifu pamoja na Makamu huyo, walilipuka kwa shangwe na kujitokeza kupongeza kiongozi huyo ambae ni miongoni mwa wawakilishi watano waliooteuliwa na Rais kuwa wajumbe wa baraza hilo.

Muda mchache baada ya kuteuliwa, wananchi mbali mbali walijitokeza kupongeza uteuzi huo kupitia mitandao ya kijamii na kumtaja Hemed kuwa ni miongoni mwa viongozi watulivu wanaoweza kuamua mambo kwa wakati.

Hemed ambae juzi aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, uteuzi ulioibua mijadala katika mitandao ya kijamii huku baadhi ya watu wakimtabiria kushika nafasi hiyo wakinasibisha na ushauri alioutoa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli alioutoa katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya mnazi mmoja mjini unguja.

Katika mkutano huo, dk. Magufuli alisema angefurahi kuona Dk. Mwinyi (aliekuwa mgombea urais kupitia (CCM)anateua Makamu wa pili wa Rais kutoka kisiwa cha Pemba ili kuimarisha umoja wa Wazanzibari.

Mteule huyo ambae hadi anateuliwa kuwa mjumbe wa baraza la wawakilishi alikuwa Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba, aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali serikalini ikiwemo ya Afisa Mdhamini wa wizara ya Biashara Pemba wakati wa serikali ya awamu ya sita iliyoongozwa na Dk. Amani Abeid Karume.

Aidha katika serikali ya awamu ya saba iliyoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein, Hemed amewahi kushika nafasi ya Mkuu wa wilaya ya mkoani katika miaka mitano ya kwanza na baadae akateuliwa mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba.