TOKYO,JAPANI

SERIKALI ya Japani inaonekana kuwa na dhamira ya kushirikiana na utawala mpya wa Marekani ili kuongoza kwa pamoja jitihada za kukuza ushirikiano wa kimataifa.

Waziri Mkuu wa Japani Suga Yoshihide alituma ujumbe kupitia mtandao wa Twitter wa kuwapongeza Joe Biden na Kamala Harris wa Chama cha Democrat kufuatia ushindi wao uliobashiriwa katika uchaguzi wa urais nchini Marekani.

Suga pia anatarajiwa kulenga kukuza uhusiano binafsi wa kuaminiana na Biden, jinsi alivyofanya mtangulizi wake Abe Shinzo na Rais Donald Trump wa Marekani.

Serikali ya Japani inapanga kufanya maandalizi na Marekani ya mkutano kati ya Suga na Biden wakati mwafaka.

Serikali ya Japani na maofisa wa chama tawala wanatumai kuwa nchi hizo mbili zitaimarisha uhusiano ili kukabiliana na changamoto za kimataifa, likiwemo janga la virusi vya corona na mabadiliko ya tabia nchi.

Hatua za kulinda masoko ya ndani na sera nyengine za utawala wa Trump zilisababisha kuvurugika kwa umoja wa dunia wakati wa matukio kama vile mikutano ya mataifa saba yaliyoendelea zaidi kiviwanda ulimwenguni, G7.

Biden anaonekana kuwa tayari kuweka msisitizo mkubwa kwa ushirikiano wa kimataifa.