NA MWANAJUMA MMANGA

JUMUIYA ya Wazee Zanzibar imempongeza Rais wa awamu ya nane wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi kwa kushinda kwenye uchaguzi mkuu na kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Akizungumza na gazeti hili katibu wa jumuiya hiyo, Amani Suleiman Kombo, alisema Dk. Mwinyi alipata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu kutokana na kukubalika kwake.

Alisema uchaguzi uliofanyika ulikuwa ni wa haki, amani na utulivu hivyo jumuiya hiyo imeridhishwa na matokeo ya kiongozi huyo. “Uchaguzi tangu unaanza mpaka unamalizika hakuna mtu yoyote aliyepigwa wala alofariki hadi hivi sasa”, alisema.

Alisema jumuiya ina matumaini makubwa kwa rais huyo mpya na kwamba ataendeleza yaliyoanzishwa na kuleta maendeleo katika kuwaunga mkono wazee katika masuala mbali mbali ya afya, pencheni jamii, na kuwawekea dirisha la kuchukulia dawa.

“Dk. Hussein ni kijana ambae hana ubaguzi na dharau kwa rika zote iwe kwa wazee, vijana na makundi mengine, hivyo matumaini ya jumuiya ni kuendelea kumuunga mkono kiongozi huyo.

“Uchaguzi umekwisha na rais mpya ameshaapishwa, hivyo ni jukumu la wananchi wote wa Zanzibar kuhakikisha wanashirikiana na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kujenga nchi yao”, alisema.

Katibu huyo alitumia nafasi hiyo kuipongeza Tume ya Uchaguzi kwa utaratibu mzuri walioweka katika vituo vya kupigia kura kuhakikisha vifaa vya kupiga kura vimepatikana kwa wakati hasa kwa watu wenye mahitaji maalum.

Pia aliwashukuru wananchi na viongozi wa dini kwa kuhubiri amani na usalama katika kipindi chote cha uchaguzi pamoja na vyombo ya ulinzi na usalama kwa kuweka nchi katika hali ya usalama.

Alisema aliwapongeza viongozi wa siasa kwa wale waliokubali matokeo yaliyotolewa na mkuu wa tume ya uchaguzi.

Pia alivipongeza vyombo mbali mbali vya habari kwa kuweza kuelimisha kudumisha amani.

Naye mlezi wa jumuiya hiyo Hashim Bakari Mzee alisema wana matumaini makubwa kwa Dk. Mwinyi katika kufanya mabadiliko makubwa Zanzibar kama anavyofanya Dk. John Pombe Magufuli kwa upande wa Tanzania bara.

Hata hivyo alisema matumaini yao kuwa Dk. Mwinyi atateua mawaziri wataofanya kazi vizuri katika kuwatumikia wananchi na watakaosimamia suala la rushwa na ubadhilifu wa mali za umma ili Zanzibar iendelee kuwa na maendeleo.

Alisema, kuna mambo mengi ambayo Dk. Mwinyi anatakiwa ayaone na kuyasimamia kwa nguvu katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.

Alisema Dk. Mwinyi aliahidi mbele ya wazanzibari atakapoingia madarakani atasimamia kwa nguvu zote suala la rushwa wabadhilifu wa mali za umma na wazembe hivyo imani yao ahadi hizo atazitimiza.