NA ABDI SULEIMAN

MRAJIS wa Jumuiya zisizo za Kiserikali Zanzibar, Ahmed Khalid Abdalla, ameitaka Jumuiya ya Community Forest Pemba (CFP) kuhamasisha vikundi vyengine juu ya suala zima la utunzaji wa mazingira kwa kuhakikisha wanapanda miti ya kutosha.

Alisema iwapo kutakuwa na vikundi vingi na vikaweza kupanda miti ya kutosha ya mikandaa, katika maeneo ambayo yako wazi maji ya bahari hayotokua na nguvu kuja juu na kuharibu mashamba ya kilimo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kumalizika kwa kikao cha pamoja baina ya ofisi ya Mrajis wa NGOs Zanzibar na viongozi wa CFP, kikao kilichofanyika Minyenyeni Gando Wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema lazima wananchi wachukue juhudi katika kunusuru maeneo maji ya bahari kutokuvamia maeneo ya kilimo, pamoja na kuingia katika majumba watu, kwa kuhakikisha wanakuwa kitu kimoja kupanda miti kwa wingi.

Alifahamisha kuwa katika miaka ya hivi karibuni suala la mabadiliko ya Tabianchi, yamekuwa yakiathiri sana shuhuli za wananchi ikiwemo maeneo ya kilimo, makaazi, hali ya hewa kubadilika, jua kali kuwaka.,

“Lazima wananchi wachukue juhudi za makusudi kunusuru maeneo ya baharini kwa lengo la kuzuia uingiaji wa maji katika maeneo huru”alisema.

Alisema imekuwa mstari wambele katika kuelimisha na kushajihisha wananchi kupanda miti ya mikandaa, pamoja na kuibua vikundi vya upandaji wa miti

Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya CFP Pemba, Mbarouk Mussa Omar, aliupongeza uongozi wa Ofisi ya Mrajis wa NGO’s Zanzibar, kuwapatia njia ya kutekeleza vikundi vizuri kwani mafanikio yakipatikana ni yawananchi wote.

Alisema CFP, ilishajihisha wananchi maeneo mbali mbali kuunda vikundi vya upandaji wa miti, kwalengo la kuhakikisha mazingira yanatunzwa ikiwa ni ardhini hadi baharini.

Alisema vikundi hivyo zimeweza kupanda miti kwa wingi, huku akitolea mfano kikundi cha Gando kilichopanda miti zaidi ya elfu 70000, katika maeneo mbali mbali kwa lengo la kurudisha asili ya maeneo yaliyowazi.

“Hili suala la uhifadhi wamazingira sio letu peke yetu, bali taasisi nyingi zinahusika sisi ndio tumeonyesha njia ila bado tunahitaji nguvu nyingi kutoka serikalini”alisema.

Hata hivyo, Mbarouk aliahidi kuendelea kushajihisha wananchi wakupanda miti ya mikoko, ili kukabiliana na athari zamabadiliko ya tabia nchi.