TUCHUKUE fursa hii kukupongeza kwa dhati Dk. Hussein Mwinyi kwa kushinda nafasi ya urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambapo unakuwa rais wa awamu ya nane wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu kuaisiwa kwa mapinduzi mwaka 1964.

Hadi kufikia hatua hiyo, katika kipindi cha miongo miwili bila shaka umepita kwenye mabonde, miteremko na hata kwenye kona kali katika jumla ya safari yako ya kisiasa.

Ushindi wa kishindo ulioupata katika uchaguzi mkuu kutoka kwa wananchi wa zanzibar, bila shaka ni ishara ya kungwa mkono na kukubalika kutoka kwa wananchi wengi hapa visiwani.

Hatua ya leo ya kulishwa kiapo baada ya kushinda kinyang’anyiro cha urais kwenye uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni, maana yake ni kukubali jukumu la kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kushirikia nao ukiwa kiongozi wao.

Hatuna haja ya kueleza mengi kwa sababu tunaelewa unajua kila kitu kuhusu Zanzibar, unajua shinda za wananchi, unajua changamoto zinazowakabili, unaishi na mambo ya wanzibari, unajua fursa zilizopo Zanzibar, lakini pia unayajua mambo yanayohitiaji kuekwa sawa.

Tunachoamini ni kwamba kazi yao itakuwa rahisi sana, hasa katika suala la kuwaletea maendeleo wananchi na kukuza uchumi wa Zanzibar, kwani mtangulizi wako Dk. Ali Mohamed Shein kwenye maeneo hayo amefanya vizuri sana.

Kazi nzuri iliyofanywa na rais mstaafu wa awamu ya saba Dk. Ali Mohamed Shein hasa ujenzi wa miundombinu, sekta ya afya, elimu na huduma muhimu za jamii bila shaka itakurahisishia kufika haraka kule tunakotaka kuelekea.

Pia safari itakuwa nyepesi zaidi na isiyochosha ingawaje ina ugumu wake, endapo amani ya nchi itaendelezwa, kwa hakika katika hili Dk. Shein alifanya vizuri tunadhani ameacha njia itakayoogoza kutufikisha tuendako.

Kama tulivyosema hatuna mengi ya kukueleza kwa sababu kila ambacho pengine tungepeswa kukuambia mwenye umeshakieleza katika mikutano yako ya kampeni.

Ilivyokuwa vizuri zaidi ni kwamba ulifanya kampeni za kisayansi kwa maana ulikutana na kila aina ya jamii ya watu wanaoishi Zanzibar na bila shaka umewasikiliza kwa makini, hivyo tunadhani maeneo hayo utayafanyia kazi.

Wananchi wamekuchagua kwa kura nyingi ni ishara ya mapenzi yao, ni ishara ya imani yao, tunadhani watafurahia na kuendelea kunufaika na matunda ya mapinduzi ya mwaka 1964 ambayo ndio msingi wa maendeleo yote ya Zanzibar.

Tunaamini sana viatu ulivyovaa vilivyoachwa na Dk. Shein havitakupwaya wala havitakubana kwani wananchi wamekupima na kuona ni saizi yako ndio maana wamekupa kura.

Tuishie kusema karibu sana Dk. Hussein Mwinyi rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa awamu ya nane na kwaheri Dk. Ali Mohamed Shein rais wa awamu ya saba, tunakuombea Mungu akupe siha na afya katika maisha yako ya kustaafu.

Dk. Shein tutakukumbuka kwa mema uliyoyafanya kwa ajili ya Zanzibar na bila shaka historia itafungua kurasa zake sio kwa yale mazuri tu uliyotuachilia lakini hata falsafa zako zitadurusiwa.