NA MADINA ISSA

ZAIDI ya watalii 500 kutoa Urusi waliingia nchini kupitia kiwanja cha ndege cha Abeid Amani Karume, ambapo ni mara ya kwanza Zanzibar kupata watalii idadi kubwa tokea kufunguliwa kwa viwanja vya ndege.

Watalii hao wamewasili kwa Shirika la Ndege la Azur Air kutoka nchini Urusi, ikiwa na watalii wenye rika tofauti ambao wengi wao ni vijana.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili kwa ndege hiyo Katibu mtendaji wa kamisheni ya utalii Zanzibar, Dk. Abdallah Mohammed Juma, alisema kuwa licha ya ujio wa wageni hao, lakini pia Zanzibar inatarajia kupokea ndege 100 za watalii ambazo zipo katika foleni ya kuja Zanzibar.

“Ndani ya miezi sita ijayo kuanzia Disemba mwaka huu ndege 100 zimeshaweka foleni ya kuja Zanzibar, ambapo ndege hizo zinatoka katika masoko mapya ya Ulaya mashariki”, alisema.

Alisema kuwa baada ya Tanzania kufanikisha kutokomeza ugonjwa wa korona, utalii umefunguka na hoteli nyingi sasa zitafunguliwa kutokana na watalii wengi kuwasili Zanzibar.

Aidha alisema uchaguzi Zanzibar umekwisha na hali ya usalama imeimarika ambapo amani iliyokuwepo imepelekea kupokea watalii wengi.

“Zanzibar njema atakae aje niwaambie vijana wale ambao ajira zao zilisitishwa mahotelini kutokana na hoteli kufungwa baada ya kukosa wageni kutokana na janga la corona sasa vijana wajiandae kufanya kazi”, alisema.

Aidha, alisema ujio huo wa wageni kwa kiwango kikubwa utapelekea hoteli nyingi kufunguliwa na kuwepo kwa ajira mpya hivyo maisha ya wananchi waliokua wakitegemea utalii sasa watayarishe bidhaa zao.

Katibu mtendaji huyo, alieleza kuwa licha ya kupokea ndege hiyo pia ndege nyengine nne kubwa zilileta wageni mwishoni mwa wiki iliyopita kutoka masoko mapya ya utalii ambayo ni Urusi, Ukraine na Kazakhstan.

Alieleza kuwa awali Zanzibar ilikuwa inategemea masoko ya utalii ya zamani ambayo ni Italia, Ufaransa, Uingereza, Marekani na Ujerumani.

Alieleza kuwa wakati dunia imepumzika kusafirisha wageni kwa sababu ya korona kamisheni ya utalii Zanzibar ilikua ikifanya kazi kubwa ya kuitangaza Zanzibar kiutalii hivyo baada ya korona kumalizika matunda sasa yameanza kuonekana kutokana na ujio wa watalii hao.

Hata hivyo, alisema kuwa wameshazungumza na jumuiya ya wawekezaji kutoka Uturuki wanatarajia kuwasili kwa ndege nyengine mpya ambayo itakuja Novemba tano mwaka huu ikiwa na watalii zaidi ya 500 kutoka Urusi.

Pia alisema kuwa shirika la ndege la Ujerumani kwa mara ya kwanza litaanza safari zake linatarajiwa kuleta ndege yake kubwa kuleta watalii Zanzibar ikitokea moja kwa moja Ujerumani ambayo itawasili Zanzibar Disemba 31 mwaka huu.