KINSHASA,DRC

KINARA wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokarsia ya Kongo Moise Katumbi amerejea katika mji mkuu Kinshasa baada ya miaka mitano na anatarajiwa kukutana na Rais Felix Tshisekedi.

Gavana huyo wa zamani wa jimbo la Katanga anakutana na rais Tshisekedi kama sehemu ya mashauriano ya kitaifa yaliyoanza Jumatatu wiki hii.

Wafuasi wa Katumbi na wanaharakati kutoka vyama vyengine walimiminika kwa wingi kwenye uwanja wa ndege wa Kinshasa kumlaki mshirika huyo wa zamani wa Joseph Kabila.

Akizungumza punde baada ya kuwasili mjini Kinshasa, Katumbu alisema ameitikia wito wa mashauriano yaliyozinduliwa na Rais Tshisekedi,kwa sababu nchi iko katika hali ya sintofahamu.

Alisema yuko tayari kufanya kazi na serikali iliyoko madarakani.

Hayo yanajiri huku kukiwa na tetesi kuwa anatafuta waitifaki wapya wa kisiasa kufuatia mzozo ulioibuka katika muungano wa kisiasa baina ya Rais Tshisekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila.

Viongozi hao wawili walikuwa wakizozana kwa muda mrefu na inaonekana hawawezi kuelewana tena.