ZASPOTI

MCHEZAJI wa soka wa zamani wa timu ya Small Simba ambae aliwahi kuwa kocha wa klabu ya Pamba FC ya Mwanza  Ali Omar Kisaka, ameiomba serikali kupanga mpango mzuri wa matumizi ya uwanja ya viwanja vya Amaan na Mao Zedong wakati ligi kuu ya Zanzibar inapoendelea.

Kisaka aliyasema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili, kwa kile alichokitaja kuwa  utumiaji mbaya wa viwanja hivyo wakati ligi kuu inapochezwa, kwa kuaharishwa michezo bila sababu za msingi.

Alisema si jambo la kupendeza wakati ligi kuu inaendelea baadaye kuaharishwa na kuwekwa mashindano ya Ndondo  au Bonanza,jambo linaloondosha hadhi na heshima ya ligi hiyo.

Alisema  utaratibu huu unaharibu ligi kwani  mashindano ama Bonanza sio sababu ya msingi ya kuahirishwa ligi kuu.

“Kuna sababu kubwa inayosababisha ligi kuu ya nchi isichezwe  kwenye viwanja hivyo,lakini sio kuharishwa kwa sababu ya Bonaza,”alisema.

Akizungumzia juu ya kuanza kwa ligi kuu ya Zanzibar  inayotarajiwa kutimua vumbi Novemba 14,alisema msimu huu ligi hiyo itakuwa ngumu na yenye mvuto kutokana na ushiriki wa timu 12.

“Msimu huu utakuwa tofauti na misimu iliyopita maana kutakuwa na ushinda mkubwa kushuka timu mbili ni jambo kubwa na kila mmoja hatokuwa tayari kushuka,”alisema.