HIVI karibuni Umoja wa Mataifa ulitangaza kwamba nchi 50 zimekubali kutekeleza azimio la mkataba wa kimataifa linalopiga marufuku silaha za nyuklia, makubaliano ambayo yanatarajiwa kuanza kufanya kazi mapema mnamo mwaka 2021.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa nchi ya Honduras imekuwa nchi ya 50 kukubali kutekeleza makataba huo wa kudhibiti uundaji wa silaha za nyuklia.

Hatua hiyo, imepongezwa na wanaharakati wanaopinga silaha za nyuklia, hata hivyo imepingwa vikali na Marekani na nchi nyengine zenye uwezo mkubwa wa nyuklia.

Makubaliano hayo yanazuia matumizi, kuunda, kuimarisha, kufanya majaribio na kuhifadhi silaha za nuklia. Hata hivyo kwa bahati mbaya sana nchi zilizosaini mkataba huo hazina uwezo wa nyuklia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres, alisema makubaliano hayo ni muhimu kwa amani na usalama duniani.

Silaha za nyuklia zina uwezo mkubwa zikiripuliwa na kusababisha maafa makubwa ya kibinaadamu na kimazingira.

Kama unakumbuka vizuri somo la kemia uliposoma atomiki na isotopes, basi hiyo ndio sehemu ya mchakato wa kutengeza bomu la nyuklia na ndio sababu mabomu ya nyuklia wakati mwingine yanaitwa mabomu ya atomiki.

Silaha ya kinyuklia hutoa kiwango kikubwa cha mionzi ambayo husababisha madhara makubwa na kwamba athari za mionzi inayotokana na mripuko wa silaha ya nyuklia zinaweza kusababisha athari hata baada ya mlipuko.

Lakini silaha hizo zimetumiwa mara mbili katika historia ya dunia, baada ya Japan kushambuliwa na mabomu ya nyuklia 1945 wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia, ambapo miji ya Hiroshima na Nagasaki ndiyo iliyokumbwa na miripuko hiyo.

Madhara yaliotokana na mionzi kutoka kwa shambulio la bomu la Hiroshima iliendelea kushuhudiwa kwa miezi kadhaa, hali ambayo ilisababisha vifo vya karibu watu 80,000.

Na bomu la pili lililodondoshwa katika mji wa Nagasaki, lilisababisha vifo vya zaidi ya watu 70,000 na tangu wakati huo silaha za nyuklia hazijawahi kutumiwa katika vita vyengine hapa duniani.

Kwa sasa nchi tisa hapa duniani zimethibitisha kuwa zinamilika silaha za nyuklia ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza, Urusi, Ufaransa, China, India, Pakistan, Israel na Korea Kusini.

Anayeweza kutengeza silaha nyuklia ni mtu yeyote aliye na uwezo wa kiufundi na kiteknolojia, lakini linapokuja suali la iwapo nchi zinaruhusiwa kutengeza silaha hizi, jibu linaweza kuwa maelezo mapana ambayo bado ufumbuzi wake haujapatikana.

Kuna suala la kujidhibiti ambalo limeangaziwa katika mkataba wa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia (NPT), lengo la mkataba huo ni kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia na kuziwajibisha nchi zitakazokiuka masharti yaliyowekwa kudhibiti uundaji wa nyuklia.

Tangu mwaka 1970, nchi 191, miongoni mwa nchi hizo Marekani, Urusi, Ufaransa na China zimetia saini makubaliano ya kuzuia uundaji silaha za nyuklia(NPT).

Nchi hizo tano zinaitwa nchi zilizojihami kwa nyuklia na ndizo zilizoruhusiwa kumiliki silaha hizo kwasababu, waliunda kabla ya kufikiwa kwa mkataba wa NPT kuanza kutekelezwa Januari 1, 1967.

Japo nchi hizo tayari zinamiliki silaha za nyuklia zimetakiwa kupunguza kiwango cha silaha hizo kulingana na mkataba huo na hazitakiwi kusalia nazo milele.

Israel ambayo haijawahi kukubali au kukana kuwa na silaha za nyuklia, India na Pakistan hazijakubali kuwa kuunga mkono mkataba huo ama kutia saini, ambapo nchi ya Korea Kaskazini ilijiondoa katika makubaliano hayo mwaka 2003.

Iran ilianza mpango wake wa nyuklia miaka ya 1950 na imekuwa ikisisitiza kwamba mpango huo ni salama.

Lakini kumekuwa na hofu huenda inatengeza kisiri silaha za nyuklia, hatua iliyofanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani na Muungano wa Ulaya kuiwekea vikwazo mwaka 2010.

Shinikizo hilo lilitoa nafasi ya kufikiwa kwa mkataba wa kimataifa wa nyuklia mwaka 2015, baina ya Iran na nchi zenye uwezo mkubwa duniani iliyotiwa saini na Iran kukubali kusitisha uzalishaji wa nguvu za nyukli, lakini rais wa Marekani Donald Trump’ alijiondoa katika mkataba huo mwezi Mei 2018.

Rais wa Iran Hassan Rouhani aliwahi kusema kuwa nchi yake haina mpango wa kuunda silaha za nyuklia.

Uhasama kati ya Marekani na Iran ulipoibuka upya mwaka huu, rais Trump alisema kuwa Iran haitaruhusiwa kumiliki silaha za nyuklia wakati wa utawala wake.

Baada ya Marekani kumuua jenerali wa Iran Qasem Soleimani mjini Baghdad, Iran ilisema haitazingatia masharti yaliomo katika mkataba wa kimataifa wa nyuklia.

Kama ilivyotajwa hapo awali, lengo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kumaliza kabisa silaha za nyuklia duniani siku zijazo, ambapo hadi kufikia sasa, idadi ya mabomu ya nyuklia duniani imepungua kutoka 70,000, mwaka 1986 hadi 14,000.

Marekani, Uingereza na Urusi zimepunguza utengenezaji wa silaha hizo hatari, lakini zipo taarifa kwamba China, Pakistan, India na Korea Kaskazini zinaaminiwa kuendeleza utengenezaji wa mabomu zaidi, kwa mujibu wa Shirikisho la Kisayansi la Marekani.

Lakini Marekani, Uingereza, Ufaransa na Urusi zilipinga kutekelezwa kwa azimio hilo la mpango wa kuzuia undwaji wa silaha za nyuklia.

Uingereza na Marekani zimesema azimio hilo halijawahakikishia usalama wa kimataifa na kwamba kuwepo kwa silaha za nyuklia kumesaidia kudumisha amani duniani kwa zaidi ya miaka 70.

Japo Marekani na Uingereza zimepunguza idadi ya mabomu miongoni mwa silaha zao za nyuklia, wataalamu wanasema nchi hizo zimeimarisha uwezo wa silaha zilizopo.

Uingereza inasadikiwa kufanya mpango wake wa nyuklia kuwa wa kisasa, nayo Marekani huenda ikatumia dola trilioni moja kuimarisha uwezo wake wa kinyuklia kufikia mwaka 2040.

Korea Kaskazini inaendelea kufanyia majaribio silaha zake na kuendeleza mpango wake wa nyuklia.

Hii inaashiria, kwamba idadi ya mabomu ya nyuklia inapungua kote duniani ikilinganishwa na miaka 30 iliyopita, hakuna uwezekano wa ulimwengu kukombolewa dhidi ya silaha hizo hatari ama kuziharibu kabisa.