NA MWAJUMA JUMA

MZUNGURUKO wa pili wa ligi Kuu ya Zanzibar unatarajiwa kuanza leo ambapo michezo miwili itachezwa katika viwanja viwili tofauti.

Michezo hiyo ambayo yote imepangwa kuchezwa majira ya saa 10:00 za jioni itachezwa katika uwanja wa Mao Zedong na Amaan.

Katika uwanja wa Amaan kutakuwa na mchezo kati ya JKU na KMKM mchezo ambao unatajwa kuwa mgumu kutokana na miamba yote miwili kutaka pointi tatu.

Itakumbukwa kwamba katika michezo yao ya awali miamba hiyo haikufanya vyema ambapo JKU ilitoka sare ya bila kufungana na Kipanga, hivyo katika mchezo wa leo itahitaji ushindi ili kujiweka vizuri.

Kwa upande wa timu ya KMKM wao ndio watakuwa wakali zaidi kwani mchezo wake wa kwanza na Zimamoto ilifungwa mabao 2-0 ambayo yalifungwa katika dakika za mwisho za mchezo huo.

Aidha katika uwanja wa Mao Zedong Mafunzo itashuka uwanjani hapo kucheza na Zimamoto, mchezo ambao nao utakuwa na ushindani wa hali ya juu.

Miamba hiyo inashuka uwanjani hapo ikiwa na pointi tatu kila mmoja na mabao  mawili, ambapo Mafunzo ushindi wake wa awali ulitokana na kuwafunga Polisi mabao 2-0.

Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo mzunguuko huo wa pili utaendelea tena Ijumaa badala ya Alkhamis ambapo michezo hiyo imeondolewa kutokana na sababu za kiutawala.

Mchezo kati ya Black Sailor na Chuoni sasa utachezwa Mao Zedong siku ya Novemba 27, wakati Malindi itacheza na Polisi siku ya Novemba 29.