NA LAILA KEIS

WANAKAMATI ya Umoja wa wazazi na walimu (UWAWA) Wilaya ya Magharibi ‘B’, wametakiwa kuwahamasisha wazazi na walezi kuwapeleka kuandikisha watoto wote waliotimiza umri wa kuanza masomo.

Msaidizi Mkurugenzi elimu ya maandalizi na msingi Baraza la Manispaa Magharibi ‘B’ Hassan Abas Hassan, aliyasema hayo wakati akizungumza na wanakamati hao huko ofisini kwake Mombasa mjini Unguja.

Alisema wanakamati hao wanajukumu la kufikisha elimu kwa jamii, ili wazazi na walezi wajitokeze kwa wingi kuandikisha watoto wao waweze kupata elimu.

“Zoezi hili linatarajiwa kuanza tarehe tisa mwezi huu hadi Januari nane mwakani, hivyo hadi kufikia tarehe hiyo tunatarajia tuwe tumetimiza malengo tulojiwekea ndani ya Wilaya yetu ya kuandikisha takribani wanafunzi elfu 10” alisema.

Aidha, alisema, kama ilivyo sera ya elimu ni kuhakikisha kila mtoto alietimiza miaka minne kuanza elimu ya maandalizi na mtoto wa miaka sita kuanza elimu ya msingi.

Alisema Mtoto aliezidi miaka zaidi ya minane atalazimika kuanza elimu mbadala, ambapo kutokana na umri wake hatochanganywa na umri mdogo, hivyo ataangaliwa kasi yake ya uwelewa ndipo walimu watashauri aingizwe darasa lipi.

Sambamba na hilo aliwataka wazazi ambao watoto wao hawana vyeti vya kuzaliwa, kuwa hiyo isiwe changamoto ya kumkosesha haki mtoto na badala yake aanze kuandikishwa, lakini itamlazimu kukitafuta cheti hicho, ili atapotakiwa tu kuanza masomo yake basi awe anacho.

Akizungumzia uwandikishaji huo, Afisa uhusiano wa Baraza la Manispaa hiyo Khairat Ali Mohamed, aliwataka wazazi kutowaficha watoto wenye ulemavu mbali mbali, badala yake wawapeleke kuandikisha ili wakapate haki yao ya msingi kama watoto wengine.

“Tuwafichuwe watoto wenye ulemavu nao wakapate elimu, yawezekana mtoto unaemficha ana kipaji na uwelewa mzuri, lakini huwezi kujua kwa kumuacha ndani” Alisema afisa huyo.

Nae mjumbe wa kamati Asya Mwinyi Juma, ambae pia ni mjumbe wa sheha wa shehia ya Kiembe Samaki, alisema ataitumia vizuri fursa hiyo kwa kupita kila nyumba kuhakikisha wazazi na walezi wote wanapeleka watoto wao kuwaandikisha.

Aidha, aliwataka wazazi kuelewa umuhimu wa watoto wao kupata elimu, hilo litawawezesha wao kutoa ushirikiano wa karibu kwa serikali, ili kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wanapata elimu ipasavyo.