TRIPOLI,LIBYA

MIILI  ya watu 17 imegunduliwa katika kaburi la umati huko magharibi mwa Libya, mkoani Tarhuna, na hivyo kufanya jumla ya miili iliyofukuliwa katika miezi ya hivi karibuni kufikia 112.

Lotfi  Tawfiq, ambaye anaongoza timu ya kuwatafuta watu waliopotea alisema miili hiyo ilibainika baada ya kufukiliwa makaburi matano tofauti.

Makaburi hayo yapo eneo la Tarhuna, mahala ambako mbabe wa kivita Khalifa Haftar, alianzisha mashambulizi yake kuelekea Tripoli.

Mwezi Juni pia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya ilitangaza kuwa iligundua kaburi la umati katika eneo lililokombolewa kutoka kwa wapiganaji wanaoongozwa na jenerali muasi, Khalifa Haftar ambaye anapata himaya ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Misri.

Tangu Aprili mwaka jana wapiganaji wa jenerali muasi, Khalifa Haftari walianzisha mashambulizi makubwa katika jitihada za kuuteka mji wa Tripoli, suala ambalo limelaaniwa na jamii ya kimataifa.

Zaidi ya watu 1,500 waliuawa katika mashambulizi hayo na wengine wasiopungua 6,000 walijeruhiwa.

Watu laki moja na nusu pia walilazimika kuwa wakimbizi,Wapiganaji hao wa Haftar wanalaumiwa kutekeleza jinai dhidi ya binadamu katika kampeni yao ya kunyakua madaraka.

Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyoko karibu na Jenerali Haftar, na nyengine ya Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO), kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.