NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

KAMPUNI ya Arena kutoka nchini Ujerumani inayojishughulisha na uwekezaji katika sekta ya nishati ya umeme, imeonesha nia ya kuwekeza hapa Zanzibar baada ya kuridhishwa na mazingira rafiki ya uwekezaji.

Mwakilishi wa kampuni hiyo, Souheil Freich alionesha azma ya uwekezaji visiwani hapa katika sekta hiyo wakati alipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika katika Ofisi ya Makamu wa Pili Vuga mjini Zanzibar, Freich alisema kampuni yake imevutiwa na mazingira rafiki ya uwekezaji yaliyopo visiwani hapa.

Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua jitihada za kuhakikisha inaimarisha mazingira ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuwa na sera nzuri.

Alisema uwepo wake umemthibitishia kwamba mazingira ya uwekezaji yaliyopo Zanzibar yanastahiki kutumiwa na wawekezaji wenye nia thabiti ya kutaka kuzisaidia jamii katika maeneo husika.

Freich alimueleza Makamu wa Pili kwamba taasisi yake imebobea katika uzalishaji wa nishati ya umeme kwa kutumia jua sambamba na utengenezaji wa mbolea.

Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla alisema ujio wa wawekezaji tofauti nchini ni ishara ya kuunga mkono mipango ya kuimarisha uchumi wa Zanzibar.

Makamu huyo aliuhakikishia uongozi huo kwamba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inahitaji utaratibu na sheria katika kuona wawekezaji hao wanakamilisha maombi yao kwa vile kamwe hakutakuwa na ubabaishaji.

Hemed alisema kwamba wapo baadhi ya wawekezaji waliowahi kuonyesha nia ya kutaka kuwekeza miradi hapa nchini, lakini walikata tamaa kutokana na urasimu wa baadhi ya watendaji wa taasisi za umma.

Alieleza kwamba uwekezaji ni eneo muhimu lenye kuongeza fursa za ajira hasa kwa vijana waliomaliza masomo sambamba na serikali kuongeza mapato.

Aliuomba uongozi wa kampuni hiyo kuangalia maeneo wanayoweza kuwekeza akitolea mfano ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati ambayo vitazalisha bidhaa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Kampuni hiyo imeshatia saini mikataba ya kuendesha shughuli za mgodi ikiwa njiani kuweka saini mkataba mwengine hivi karibuni katika jitihada za kuwekeza miradi yake nchini Tanzania.