NA ZAINAB ATUPAE

BENCHI la ufundi la klabu ya Malindi SC, limeahidi kufanya mabadiliko makubwa ya timu yao.

Malindi inayoshiriki ligi kuu ya Zanzibar ambapo msimu uliomalizika ilijikusanyia pointi 37 iliyoongozwa na Mlandege kwa pointi 68.

Akizungumza na gazeti hili kocha mkuu wa timu hiyo Mohamed Badru Juma, alisema mabadiliko hayo yanatokana na usajili alioufanya kwenye dirisha kubwa la usajili lililomalizika hivi karibuni.

“Nataka mtambue kuwa msimu tunachotaka ni kuwa kitu kimoja,ili kufikia malengo yetu,”alisema.

Alisema wamefanya usajili wa aina yake,huku akiamini kuwa watafanya vyema kwenye mashindano yao.

Aliwambia viongozi,wachezaji,wadau na wazawa wa timu hiyo kuendelea kuiunga mkono klabu yao kuhakikisha wanarejesha hamasa ya timu.

“Timu nilipoichukuwa ilikuwa ipo hali mbaya na ilikaribia kushuka daraja,lakini nina imani kubwa kwa mashirikiano tunayoyapata basi tutafikia malengo,”alisema.

Timu ambazo zitashiriki ligi kuu msimu huu ni Mlandege, KVZ, JKU, KMKM, Zimamoto, Mafunzo, Kipanga, Polisi, Hard Rock, Malindi, Chuoni na Black Sailor.