NA LAILA KEIS

BARAZA la Manispaa Magharibi ‘B’ lipo katika zoezi la uhakiki wa wajasiriamali kwa lengo la kuwapatia vitambulisho maalum vitakavyowawezesha kuendesha vyema shughuli zao za biashara.

Mkurugenzi msaidizi mipango utawala na fedha Baraza la Manispaa Magharibi ‘B’, Ameir Ali Haji, aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa gazeti hili huko ofisini kwake Mombasa.

Alisema zoezi hilo ni moja ya utekelezaji wa agizo la serikali la kuwatengezea wajasiriamali hao vitambulisho ambavyo vitakuwa ni vya mwaka mzima.

“Hii ni hatua ya kwanza huku tukisubiri kanuni na muongozo kutoka serikalini, ili tuweze kulifanikisha hili bila kuwakwaza wafanya biashara na sisi tupate fursa ya kuingiza mapato katika manispaa yetu” alisema.

Alisema walengwa zaidi wa zoezi hilo ni wafanyabiashara wadogo wadogo kama wauza matunda na samaki juu ya meza, ambao walikua hawakati leseni kutokana na ukubwa wa biashara zao.

Hivyo alisema wafanyabiashara hao watatakiwa kulipia kipande hicho kwa ajili ya ada, ili kuondoa utaratibu ulokuwepo sasa wa kuwatoza shilingi elfu moja kwa siku.

Aidha alisema kwa kufanikisha zoezi hilo, baraza limeshaweka vikao na watu wa mapato ili kujua ni namna gani wanaweza kuendesha zoezi hilo ipasavyo.

Alisema zoezi la kuandaa vipande hivyo pia litasaidia suala zima la ukusanyaji wa mapato kwa mwaka huu na miaka ijayo iende kwa ufanisi uliotarajiwa.

Naye Hamisi Visenti mfanyabiashara ya mahindi maeneo ya Mwanakwerekwe alisema kwa upande wake amefurahishwa na utaratibu huo, kwani utawaondoshea usumbufu na kupitia vipande hivyo watatambulika rasmi.