NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia viongozi watatu wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe  kwa madai ya kuwashawishi vijana kuandamana.


Akizungumza jana  Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema mbali na viongozi hao, watu kadhaa pia wanashikiliwa.
Mbali na Mbowe viongozi wengine waliokamatwa ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema pamoja na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Boniface Jacob.

“Tunawashikilia kwa kuwa wanashawishi vijana kuandamana ili kutekeleza vitendo vya kiuhalifu, na kinara mmoja aitwaye Issack Lulandala amekamatwa akiwa  anahamasisha vijana kuandamana.”
“Baada ya mahojiano alikiri kupewa kazi hiyo na viongozi wa Chadema, ikiwa sambamba na kuhatarisha usalama wa raia na mali zao. Leo walipanga kuwatumia vijana kuchoma moto miundombinu na masoko,” amesema Mambosasa.


Amesema usiku wa kuamkia jana polisi walifanya msako kuwakamata wanaodaiwa kuwashawishi  vijana kushiriki maandamano, kuharibu mali kama kuchoma magari, kuchoma visima vya mafuta, kuchoma matairi, ili kuvuruga amani na kuleta taharuki ili shughuli za wananchi zisimame.
Amedai wanaoshawishiwa ni vijana ambao hawana woga na wavuta bangi na waathirika wa dawa za kulevya.

Mambosasa amesema, “hawakutoa taarifa kwa polisi na badala yake wanahamasishana ili kufunga barabara za jiji. Sisi kama polisi tunaingia hapo kuhakikisha hakuna  atakayeruhusiwa kufanya maandamano na mikusanyiko isiyo halali.”