NA MARYAM HASSAN

MKUFU mmoja pamoja na pete nne vyote vikiwa vya silva, vimewapeleka rumande Vuga vijana wawili wakaazi wa wilaya ya Mjini Unguja.

Vijana hao ni Haji Khamis Haji (22) mkaazi wa Mboriborini na Abubakar Abdalla Mohammed (28) mkazi wa Shauri moyo, ambao wamepelekwa rumande na mahakama ya mkoa Vuga baada ya kunyimwa dhamana.

Mapema wote hao kwa pamoja, wamepandishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Makame Mshamba Simgeni na kusomewa shitaka la wizi.

Shitaka hilo walisomewa chini ya vifungu vya 251 (1) na 258 vya sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Hati ya mashitaka kwa washitakiwa hao ilisomwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Asma Juma.

Hati hiyo inaeleza kuwa, washitakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Juni 30 hadi Julai 1 mwaka jana majira ya saa 6 na 7 za usiku, huko Amani Fresh wilaya ya Mjini mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Ilidaiwa kuwa, wakiwa katika nyumba inayomilikiwa na Suleiman Mgeni Ali, waliiba TV moja flat scrini ya nchi 24 rangi nyeusi, kinga’muzi cha Zanzibar Cable, Home theater moja, pete nne pamoja na cheni moja vyote vikiwa ni vya silva.

Vitu vyengine ni kofia moja aina ya kapelo, kofia ya kiua moja, viatu vya buti pea nne, DVD moja aina ya singsung rangi nyeusi, fedha taslimu EURO 400, vitu vyote hivyo vikiwa na thamani ya shilingi 3,861,000 kwa makisio mali ya Suleiman Mgeni.