ZAINAB ATUPAE NA ABOUD MAHMOUD

WAWAKILISHI wa Zanzibar kwenye mashindano ya kimataifa, Mlandege na KVZ, wameelezea matumaini yao juu ya mashindano hayo.

Mabingwa  wa soka visiwani Zanzibar, Mlandege FC inayoshiriki mashindano ya kombe la klabu bingwa Afrika, imesema inatambua ugumu wa mashindano hayo ila imejinga.

Akizungumza na Zanzibar Leo kocha mkuu wa timu hiyo, Abdulmutik Haji  ‘Kiduu’ alisema wachezaji wake wamejipanga vyema kuhakikisha wanafanya vyema.

Alisema mpaka hivi sasa amewasilisha maombi kwa uongozi wa timu hiyo kupatiwa mechi ya kirafiki kutoka nchi yoyote, ambayo ina kiwango kama cha timu ambayo watacheza nayo katika mashindano hayo.

Kiduu alisema endapo watapata mechi hiyo itawasaidia kufanya vizuri.“Nimepeleka maombi kwa uongozi wa timu ili kutupatia mechi ya kirafiki kwa timu kama Sudan,Misri,Morocco au nchi nyengine ambayo ina kiwango na timu tutakayokutana nayo,lakini pia tumeomba kupatiwa kambi nje ya Afrika ili wachezaji waweze kubadilisha mazingira,”alifafanua.

 Hivyo Kiduu amewaomba mashabiki wa Mlandege pamoja na viongozi wa serikali na wadau wa michezo kuisaidia timu hiyo kwa hali na mali ili iweze kufanya vyema katika mashindano hayo.

Mlandege FC inatarajiwa kushuka dimbani mwishoni mwa mwezi huu kwa kucheza na timu ya ES Sfaxien ya nchini Tunisia kuwania kombe la klabu bingwa Afrika.

 Nao wawakilishi wa Zanzibar katika kombe la Shirikisho Barani Afrika timu ya (KVZ),wamesema licha ya kupangiwa na timu ngumu katika  mashindano hayo, lakini  watacheza kwa kujituma ili kufanya vyema.