Ni mtoto wa msanii mahiri, marehemu Issa Matona
Ameizunguka dunia kupitia fani hiyo

ZASPOTI
‘MWANA wa nyoka ni nyoka’ ni usemi wa kiswahili ambao umekua maarufu ndani ya vinywa na masikio ya watu wengi, unaofananisha kwamba kiumbe chochote lazima kizae kinachofanana nacho, na kamwe haiwezekani kuwa Simba kuzaa kuku au mbuzi.
Naunasibisha msemo huu na msanii marufu nchini Tanzania, Mohammed Issa Matona ambae amejizolea sifa nyingi kupitia fani yake ya muziki wa taarab.


Mohammed ni mtoto wa aliyekua msanii nguli wa fani ya utunzi na uimbaji wa nyimbo za taarab asilia, Issa Matona Haji ambae ameshatangulia mbele ya haki na bado nyimbo zake zinaendelea kupendwa hadi hivi sasa.
Mohammed ni msanii ambaye kila siku zinavyokwenda anazidi kujizolea umaarufu kutokana na kuwa na vipaji vingi ndani ya fani ya muziki ikiwemo kupiga ala zote za taarab asilia na nyenginezo.


Lakini mbali ya kuwa na ujuzi huo, Motona anajivunia kuwa na vipaji vya utunzi wa nyimbo za taarab, muziki pamoja na uimbaji ambapo nyimbo zake zimeweza kumtangaza vyema yeye pamoja na fani kwa ujumla.
Kutokana na kubobea kwake, nilibahatika kufanya mazungumzo na gwiji huyo na kunielezea sababu za kujiunga katika fani hiyo, alipofikia na matarajio yake ya baadae.
“Fani ya muziki wa nimerithi kutoka kwa marehemu baba yangu mzazi yeye alikua msanii wa kutunga nyimbo za kuimba”.


“Kutokana na maji hufuata mkondo mimi na ndugu yangu Abdulhakim tukajitumbukiza huko”, alisema.
Kama kawaida ya wasanii wengi, Matona, anasema, alianza fani ya sanaa akiwa mdogo wakati anasoma madrasa kwa kughani kasida pamoja na kwaya za skuli.
Anasema, alikuwa kiongozi wa kusoma kasida katika madrasa mbali mbali alizokuwa akisoma kila wanapokwenda kwenye shughuli na kumsababishia kuanzia vizuri katika fani hiyo.


Lakini kwa upande wa mitaani msanii huyo nguli anasema alikua anashirikiana na wenzake wakipiga ngoma kwa kutumia mabati ya maziwa ka kutumia maplastiki wakiimba nyimbo zinazoimbwa na baba yake.
“Nilianza fani hii mdogo, ni safari ndefu niliyopitia hadi kufikia hapa nilipo sasa”, alieleza.
Anasema baada ya hapo alijiunga na kikundi cha msanii na mwanasiasa maarufu visiwani humu, Borafya Silima ambapo katika kipindi cha sikukuu walikua wakifanya maigizo katika kiwanja cha kufurahishia watoto Kariakoo na Mnazimmoja.


Anasema akiwa katika kikundi hicho, alikuwa muigizaji kama shetani wa mzimu wa jini kisiki ambae nafasi hiyo ilikua ikiigizwa na Borafia Silima wakati huo.
“Mwaka 1982, nilihamishiwa mkoani Morogoro kwa ajili ya masomo kutokana na hapa nilikua sisomi, lakini, nilipofika huko wakati nasoma skuli niliingizwa katika katika kikundi cha Brass Band na kua kiongozi kutokana na kipaji changu nilichokua nacho”.
Matona anasema sababu zilizomfanya ajiunge na taarab akiwa anasoma skuli, alikosana na mwalimu mkuu Mkoani Morogoro na aliamua kurudi kumsalimia baba yake kutokana na muda mrefu kutoonana.


Anasema akiwa jijini Dar es Salaam siku moja marehemu baba yake alikodiwa kupiga harusi na nyumbani kwake hakua na mke ilimlazimu amchukue mwanawe aende nae .
“Tulipokwenda kwenye harusi mpiga ngoma wake hakuja, alikua anaumwa na tumbo, shughuli ikawa na mashaka nikamuonea huruma nikamfuata kumwambia mimi naweza akanitolea ukali na nikamshikilia”.
“Mwisho wapigaji wake wakamwambia mzee mtoto anajiamini, wakamwambia mtoto akilia wembe mpe,akatoa ukali na kuwaambia fanyeni nyie”.


“Wakanipa ngoma nikawaambia nipige mipigo gani wakanifanifahamisha na ilikuwa chakachacha na kumbwaya na nikapiga vizuri nilitunzwa sana, huo ndio ulikua mwanzo wangu wa kujitumbukiza kwenye taarab,”alisema.


Anasema baada ya hapo, mwaka 1987 baba yake alikua na kikundi cha kidumbak na huku akiimba bendi ya taarab ya Tandika na alikua anamfuata na kupiga ngoma, hapo alianza kuona ala na kujifunza ‘tashkoto’ ambayo inatumika katika taarab Mombasa, Kenya.
Anasema baadae alianza kujifunza ala ya ‘accordion’ na akawa anapiga ngoma, ‘tashkoto’ na baadae alijifunza kupiga ‘bass gitaa’ ambavyo alikua akiwaangalia wapigaji na baadae kuanza kujifunza kutwa nzima.


“Nilikua nawaangalia wapigaji na baadae nikawa najifungia chumbani napiga huku naimba nyimbo zake ndipo nilipojua kupiga ala mbali mbali mpaka nikajua hapo tena nikasahau mambo ya kusoma na nikajiunga na muziki nikawa nalipwa shilingi 300 tu ingawa baba yangu alinilazimsiha nirudi skuli”, anasema.


Matona anasema kikundi cha taarab cha Ghazi kilimuona anapiga rika na kumpenda na kumshawishi na na kuwajibu kwamba amekatazwa na mzazi wake kujihusisha na muziki, lakini, alishikiliwa na wazee akiwemo Abdulaziz Yussuf, Kassim Said Nassor wote wakiwa marehemu na ikamlazimu akubali.

INAENDELEA TOLEO LIJALO