NA NASRA MANZI

MWAKILISHI wa Jimbo la Makunduchi, Haroun Ali Suleiman, amewataka wanafunzi waliofaulu daraja la kwanza kwenye mitihani yao ya Taifa kidatu cha Sita mwaka huu  ,kufanya jitihada katika masomo kwa lengo la  kupata viongozi bora na wadilifu  katika nchi.

Akizungumza na wazee pamoja na  wanafunzi, baada ya kuwazawadia fedha taslimu kwa kila mmoja ,hafla iliyofanyika katika ofisi za Wilaya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema lengo kuwapa nguvu katika masomo   ikiwa ni ahadi yake aliyoitoa wakati wanafunzi hao wakifanya mitihani daraja la kwanza huko Makunduchi.

Pia alisema nchi inahitaji wasomi na viongozi imara watakaowajibika na ndio sababu serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha sekta ya elimu.

“Vijana mmepata ‘division one’ mkaitumie taaluma vizuri lakini msisahau kuwa wazalendo katika nchi yenu na msije kuwangusha someni na msaidie na wengine” alisema.

Sambamba na hayo, aliwataka wanafunzi hao kuwa wadilifu na kupenda Serikali yao pamoja na viongozi kwa  kutobadilisha mawazo yao katika kutafuta  elimu.

Ofisa wa Mipango Wilaya ya Kusini Unguja, Ali Haji Ali, alisema watumie fursa za kielimu kwa ajili ya kuwasaidia katika kupata maendeleo na kujiepusha na viashiria vitakavyo waharibia masomo yao.

Nae, Ofisa wa Elimu, Mussa Nahodha Makame, alisema ipo  haja kwa wanafunzi kufanya jitihada katika masomo, ili kufanya vizuri kwa lengo la kuja kutumikia taifa katika sekta mbali mbali katika nchi.

Diwani wa Wadi ya Muyuni, Mustafa Mohamed Haji, aliwataka vijana hao kuendelea na ujasiri na kutovunjika moyo katika masomo, ili kusudi kufikia malengo waliokusudia.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Miraji Haji Mshamba, alimpongeza mwakilishi huyo kwa uweledi alionesha na kuwapatia maendeleo wanafunzi katika sekta ya elimu.

Pia alisema wamefarajika kwa kuwawezesha wanafunzi katika elimu, jambo ambalo limewapa nguvu ya kupiga hatua katika masomo yao.