KABUL,AFGHANISTAN

MKUU wa Shirika la Kujihami la NATO, Jens Stoltenberg, ameonya kwamba hatua ya Marekani kuondoa kwa ghafla wanajeshi wake nchini Afghanistan kunaweza kuigeuza nchi hiyo kuwa jukwaa la magaidi wa kimataifa.

Kauli ya Stoltenberg ilitolewa muda mchache kabla ya wizara ya ulinzi ya Marekani kutangaza kwamba itapunguza kwa kiasi kikubwa wanajeshi wake nchini Afghanistan, ambako wanasaidiana na kikosi cha NATO, na Iraq na kubakisha wachache baada ya takribani miaka 20 ya vita.

Katibu mkuu huyo wa NATO alisema makundi ya kigaidi ya IS yanaweza haraka kurejesha dola lao walilolipoteza Iraq na Syria kwenye ardhi ya Afghanistan, endapo Marekani itaondosha wanajeshi wake bila mipango inayowashirikisha wengine.

Hili ni tamko la nadra kwa mkuu huyo wa NATO, ambaye kawaida huwa hamkosoi hadharani Rais Trump wa Marekani, ambaye ndiye aliyechukuwa uamuzi huo.